SALAMU ZA MWAKA MPYA ZA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA MHESHIMIWA DKT. JAKAYA MRISHO KIKWETE KWA WATANZANIA,
TAREHE 31 DESEMBA, 2013
Utangulizi
Ndugu zangu;
Watanzania Wenzangu;
Niruhusuni
nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema, kwa kutujalia uzima
mpaka kufika na kuiona siku hii ya leo
ya kuuaga mwaka 2013 na kuukaribisha mwaka 2014. Wapo ndugu, jamaa na marafiki zetu wengi
ambao hawakupata bahati tuliyoipata sisi kwa vile wametangulia mbele ya haki. Tuendelee kumwomba Mola wetu awape mapumziko
mema na azilaze roho zao mahali pema peponi. Ameen.
Hali ya Usalama
Ndugu Wananchi;
Tunaumaliza mwaka 2013 nchi yetu ikiwa salama na tulivu.
Mipaka iko salama na ile hali ya wasiwasi tuliyokuwa nayo kwa nyakati fulani mwaka
huu sasa haipo tena. Uhusiano wetu na majirani ni mzuri na tutaendelea kufanya
kila tuwezalo kuhakikisha kuwa hali inaendelea kuwa hivyo au hata kuwa bora
zaidi mwaka 2014 na daima dumu.















































