Shinyanga
Katika hali isiyokuwa ya kawaida wakazi wa jimbo la Msalala
wilayani Kahama mkoa wa Shinyanga wamemuomba mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya
bunge ya ardhi, maliasili na mazingira, James Lembeli(Pichani kushoto) kumuomba radhi Mbunge wa
jimbo lao Ezekiel Maige(Pichani Kulia) kutokana na kashifa aliyomzushia na kusababisha apoteze
uwaziri wake.
Madai ya wakazi wao yametolewa siku chache baada ya Lembeli
ambaye pia ni mbunge wa jimbo la Kahama kupokelewa kama shujaa mara baada ya
kurejea kutoka bungeni akipongezwa kwa kazi aliyoifanya na kusababisha
kuwajibishwa kwa mawaziri wanne wanaotuhumiwa kushindwa kuwajibika katika
operesheni tokomeza ujangili.
Wakazi hao walisema wamelazimika kumtaka Lembeli amuombe
radhi Maige ili amsafishe mbunge wao huyo kutokana na tuhuma kali alizomzushia
wakati akiwa waziri wa maliasili na utalii akimtuhumu kwa madai yasiyokuwa na
ukweli kwamba alihusika na utoroshaji wanyamahai kwenda nje ya nchi kinyume cha
sheria.
Walisema madai yao hayo yanatokana na ukweli alioukiri
Lembeli bungeni wiki iliyopita wakati akiwasilisha taarifa ya kamati yake
iliyochunguza vitendo viovu vilivyotendwa na askari mbalimbali waliokuwa
wakitekeleza operesheni tokomeza ambapo alikiri kutohusika moja kwa moja kwa
waziri mwenye dhamana, Khamis Kagasheki.
Akifafanua mmoja wa wakazi hao waliozungumza na Majira jana
aliyejitambulisha kwa jina la Masanja Joseph alisema katika taarifa yake
bungeni wiki iliyopita Lembeli alimsafisha aliyekuwa waziri wa wizara hiyo
(Kagasheki) akidai hakuhusika katika kashfa ya wananchi kutendewa vitendo viovu
katika operesheni hiyo bali watendaji wake.
Joseph alisema Lembeli katika taarifa yake bungeni alidai
watendaji ndani ya wizara ya maliasili wakiongozwa na katibu mkuu wao Maimuna
Tarishi ndiyo wanaostahili lawama na waziri Kagasheki hahusiki moja kwa moja na
tuhuma hizo hali ambayo amedai imewashangaza wakazi wa jimbo la Msalala kwamba
imekuwa ni tofauti na alivyohukumiwa Maige wakati huo.
“Taarifa ya Lembeli kutaka kumsafisha Kagasheki inaonesha
jinsi gani hata mbunge wetu Maige hakuhusiki moja kwa moja na tuhuma
alizozushiwa alipokuwa waziri wa wizara hiyo, maana wakati huo Lembeli
alielekeza moja kwa moja tuhuma zilizotolewa kwa mbunge wetu (Maige), leo
anadai waziri kama waziri hawezi kuhusishwa moja kwa moja, hii ni ajabu,”
“Sasa kutokana na kukiri huko ni wazi wakati huo Lembeli
hakumtendea haki Maige kwa vile alimshambulia moja kwa moja yeye kama waziri na
kushinikiza awajibishwe peke yake katika nafasi aliyokuwa nayo hali ambayo kwa
majibu yake hayo ya juzi imeonesha alikuwa na chuki zake binafsi dhidi ya
mbunge wetu,” alisema Joseph.
Hata hivyo Joseph alikumbusha hoja za wabunge wa majimbo ya
Nyamagana, Ezekiel Wenje na Mchungaji
Peter Msigwa waliolishauri bunge wakati wa mjadala wa taarifa ya utoroshwaji wa
wanyamahai kwenda nje ya nchi ambapo walipinga kitendo cha Maige kuhukumiwa kwa
hukumu ya wengi (mob justice) Mkazi
mwingine wa kata ya Isakajana aliyejitambulisha kwa jina moja la Mwanamange
alisema baada ya Lembeli kufanikiwa kuwaondoa mawaziri wawili katika wizara
moja kuna kila sababu na yeye achunguzwe usafi wake katika kazi hiyo
anayoifanya huenda kuna kitu anachonufaika nacho kwa maslahi ya watu wengine au
yeye binafsi.
“Mimi siyo msomi sana, lakini kitendo cha Lembeli
kuwawajibisha mawaziri wawili ndani ya wizara moja kimenishitua sana, lakini
kwa Maige ndiyo nilibaki na maswali mengi bila ya majibu, maana huyo bwana
(Maige) hakupewa nafasi yoyote ya kutoa utetezi wake bungeni, aliwajibishwa
moja kwa moja,” “Kwenye taarifa ya
Lembeli juzi kuhusiana na operesheni tokomeza ameonesha wazi kutaka kumtetea
Kagasheki, hii inatia hofu ndani ya akili yangu, vipi huyu alimsulubu moja kwa
moja na kumnyima nafasi ya utetezi, lakini mwingine amtetee kwa nguvu zote na
kutaka kumtupia mzigo huo katibu mkuu wa wizara?” alihoji Mwanamange.
Alisema binafsi anamshauri Lembeli achukue maamuzi magumu ya
kumuomba radhi Maige kutokana na kitendo alichomtendea kwani wakati
akimwajibisha alimwajibisha peke yake wakati tuhuma yake ingewagusa pia watu
wengi wakiwemo maofisa usalama wa Taifa walioruhusu ndege ya kijeshi kutoka nje
ya nchi kuondoka nchini ikiwa na wanyamahai.
No comments:
Post a Comment