Friday, September 27, 2013

JAJI WARIOBA AANIKA MAZITO

Wakati wananchi wa kada mbalimbali wakishinikiza Rais Jakaya Kikwete kutokusaini Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba 2013, kwa maelezo kuwa una kasoro, Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba naye amesema sheria ina upungufu.

Warioba alisema jana kwamba ni jambo la kushangaza sheria hiyo kueleza kuwa tume hiyo itavunjwa baada ya kukabidhi Rasimu ya Katiba kwenye Bunge Maalumu la Katiba, wakati huohuo ikieleza kuwa itahusika tena kusimamia utoaji wa elimu ya kura ya maoni.

Kauli hiyo ya Warioba imekuja wakati vyama vya NCCR Mageuzi, Chadema na CUF, vikifanya mikutano nchi nzima kuwashawishi wananchi kupinga kile wanachokiita hujuma dhidi ya upatikanaji wa Katiba Mpya.

Sheria hiyo ambayo Warioba amesema ina upungufu, muswada wa marekebisho yake ulijadiliwa na kupitishwa wa wabunge Septemba 6, mwaka huu katika Mkutano wa 12 wa Bunge Mjini Dodoma, ikiwa ni baada ya kubadilishwa kwa baadhi ya vifungu na hivi sasa Rais Kikwete anasubiriwa kuusaini ili iwe sheria kamili. Akizungumza na waandishi wa habari jana, Jaji Warioba alisema: “Mwisho wa kazi ya tume ni baada ya kukabidhi rasimu, hilo ni tatizo. Maana tume itakuwa imeshavunjwa, sasa itafanyaje kazi ya kutoa elimu kwenye kura ya maoni?”


KENYA YAMSAKA SAMANTHA

Polisi wa kimataifa Interpol, wamemuweka mwanamke aliyeshukiwa kuongoza mashabulizi ya kigaidi nchini Kenya raia Muingereza Samantha Lewthwaite, kwenye orodha ya watu wanaosakwa sana duniani.

Hatua hii ni kutokana na ombi la serikali ya Kenya kwa Interpol.Bi Lewthwaite, mwenye umri wa miaka 29, ni mjane wa mlipuaji aliyefanya shambulizi la kujitoa mhanga mjini London Uingereza mwezi Julai mwaka 2005 anajulikana kama "white widow", na amehusishwa na kundi la kigaidi la Al Shabaab nchini Somalia.

Polisi wa Interpol hata hivyo hawakuhusisha hatua ya kumsaka Samantha na shambulizi la kigaidi dhidi ya jumba la maduka la Westgate mjini Nairobi lililowaua watu 67.

Hata hivyo, hatua hii ya kumsaka Bi Lewthwaite inakuja punde baada ya shambulizi hili la kigaidi nchini Kenya. Al-Shabab ilikiri kufanya mashambulizi hayo yaliyotokana na kutekwa kwa jengo la Westgate na kisha kutekwa kwa raia wa kawaida waliokuwa ndani ya jengo hilo kwa siku nne.


ATUPWA JELA KWA KUTOA MUZIKI WA MATUSI


Msanii wa kizazi kipya nchini Tunisia, Ahmed Ben Ahmed, anayejulikana kwa jina la kiusanii, Klay BBJ, amehukumiwa jela kwa miezi sita kwa kuwatusi maafisa wakuu kupitia kwa muziki wake. Mahakama ilitupilia mbali kesi yake ya rufaa baada ya yeye na mwanamuziki mwenzake kupatikana na hatia mwezi jana ya kuwatusi maafisa wakuu katika tamasha la muziki eneo la Hammamet.

Wawili hao awali walihukumiwa bila ya wao kuwepo mahakamani kutumikia kifungo cha miezi 21 lakini hukumu hiyo iliondolewa. Weld El 15, aliyepatikana na kosa kwa kuimba wimbo wake huo, kuwa 'Ploisi ni Mbwa', hakukata rufaa na sasa yuko mbioni.


Wednesday, September 25, 2013

MWANAMKE AONGOZA SHAMBULIZI LA KIGAIDI

Huku mapambano yakiwa yamepamba moto, anayedaiwa kuwa Kiongozi wa kundi la magaidi lililovamia jengo la kibiashara la Westgate, Samantha Lewthwaite inadhaniwa kuwa ameuawa.

Lewthwaite, ambaye anaitwa kwa jina la utani la ‘Mjane Mweupe’ anadaiwa kuongoza shambulizi hilo lililosababisha vifo vya watu 62 na kujeruhi wengine 170 mjini Nairobi.

Kwa mujibu wa gazeti la Daily Mail la Uingereza, mwanamke huyo inasemekana aliuawa juzi usiku na wanajeshi wa Kenya wanaoshirikiana na maofisa wa Shirika la Ujasusi la Israel (Mossad) na wale wa Shirika la Upelelezi la Marekani (FBI).

Gazeti hilo lilieleza kuwa mwanamke huyo ambaye ni mjane wa mlipuaji wa kujitoa muhanga, Jermaine Lindsay, aliuawa pamoja na magaidi wengine watatu.


KENYA YAOMBELEZA KWA SIKU 3

Kenya inaanza siku tatu za maombolezi ya kitaifa kwa waathiriwa wa mashambulizi ya kigaidi yaliyofanyika katika jengo la kibiashara la Westgate mjini Nairobi.

Rais Uhuru Kenyatta pia ameseama kuwa bendera zitapepershwa nusu mlingoti kwa heshima ya waliopoteza maisha yao katika mashambulizi hayo.

Watu 67 wameuawa ikiwemo wanajeshi kadhaa wa usalama, ingawa kuna hofu kuwa idadi ya waliofariki huenda ikaongezeka.

Maafisa wa uchunguzi wa kimataifa wanaungana na wale wa Kenya kujaribu kuondoa mili ambayo imenaswa kwenye vifusi vya jengo hilo ambalo sehemu yake iliporomoka jana, nia ni kujaribu pia kutambua uraia wa washambulizi hao.


Tuesday, September 24, 2013

MAGAIDI WAWILI WAUAWA, IDADI YA VIFO YAFIKIA 62

Wakati magaidi wawili wakiwa wameuawa, Serikali ya Kenya imesema idadi ya watu waliokufa katika tukio la kigaidi kwenye maduka makubwa ya Westgate, Nairobi imefikia 62.

Akizungumza na waandishi wa habari jana mchana, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Kenya, Joseph Ole Lenku alisema watu waliojeruhiwa ni 175 baada ya magaidi hao kuvamia eneo hilo la maduka tangu Jumamosi iliyopita.

Ole Lenku alisema pia kuwa askari 10 wamejeruhiwa katika operesheni hiyo inayowahusisha maofisa wa Shirika la Ujasusi la Israel (Mossad), wale wa Shirika la Upelelezi la Marekani (FBI)Alisema askari waliojeruhiwa na raia wanatibiwa katika hospitali mbalimbali za Nairobi.

Magaidi wawili wauawaAlisema magaidi wawili waliuawa na vikosi vya usalama huku mapambano yakiendelea. Alisema waasi hao wamebanwa baada ya vikosi vya ulinzi na usalama kudhibiti sehemu kubwa ya jengo hilo. Magaidi hao wanaoaminika kuwa wafuasi wa kundi la Al-Shabaab la Somalia walivamia jengo hilo la ghorofa nne ambalo lina maduka ya kifahari na kuua, kujeruhi na kuwashikilia wengine mateka.


VIKOSI VYA KENYA VADHIBITI JENGO WESTGATE

Hatimaye vikosi vya usalama nchini Kenya vinasema vimelidhibiti jengo zima la Westgate mjini Nairobi, ikiwa ni zaidi ya siku tatu baada ya jengo hilo kuvamiwa na wanamgambo.Milipuko ikifuatiwa na milio ya risasi imesikika kutoka ndani ya jengo hilo asubuhi ya leo huku duru zikisema kuwa vikosi vya usalama vinaelekea kukamilisha operesheni hiyo.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari, magaidi sita waliokuwa wamesalia wameuawa huku wengine watatu wakiuawa hapo jana.Serikali imesema zaidi ya watu 60 wameuawa na wengine zaidi ya 170 kujeruhiwa katika shambulio hilo ambalo Al shabaab imekiri kulitekeleza.

Wizara ya mambo ya ndani imesema wanajeshi wanaendelea kulisaka jengo zima la Westgate kutoka gorofa moja hadi nyingine kuhakikisha kwamba hakuna mateka aliyesaliaWakati huohuo, waziri wa mambo ya nje amesema kuwa wawili kati ya wanamgambo watatu waliofanya shambulii hilo ni raia wa Marekani pamoja na mwanamke muingereza.


CHRISTINA AVALISHWA PETE YA UCHUMBA

Muimbaji Christina Milian ameonesha pete ya uchumba aliyovalishwa na mpenziwe mpya Jas Prince, na akaliambia jarida la People kuwa "Hakika nimezama kwenye penzi la mtu niko katika mahusiano yenye furaha sana, mahusiano madhubuti jambo ambalo ni kubwa, na ananisapoti sana hakika tunaangalia mbele"



KUNGUNI WAVAMIA BUNDA

WAKAZI  wa Kijiji cha Kunzugu  kata ya Kunzugu wilayani Bunda  wameiomba Idara ya afya kuwanusuru na uvamizi wa wadudu aina ya  Kunguni  katika nyumba zao zenye kaya 399.

Wakazi hao wametoa  ombi hilo jana kwa mbunge wa jimbo la Bunda Stephen Wasira katika mkutano wa adhara kijijini hapo  ambapo walieleza  kuwa kuna kunguni wa kutisha hasa baada ya idara ya afya  kunyunyuzi  katika nyumba hizo  dawa ya kuua mbu.

Walidai kunguni hao wamevamia nyumba zao na kuishi kwenye vitanda, mashuka, meza, viti, nguo na kila kona ya nyumba ambapo wametumia  kila njia ya kuwaangamiza  bila ufanisi.


KEYSHIA COLE NDOA YAKE YAYUMBA

Ndoa ya muimbaji Keyshia Cole inaonekana kuyumba baada ya wawili hao kuthibitisha kupitia ujumbe uliotumwa katika mitandao ya kijamii.Keyshia Cole na mumewe Daniel Gibson wanapitia kipindi kigumu cha ndoa yao na wamekuwa wakiandika ujumbe unaonesha kutengana.

Keyshia aliandika kwenye mtandao wa Instagram kuwa "Mji wa  Cleveland ulikuwa mtamu kwa mumewangu na mimi pia tumeacha kumbukumbu kubwa hapa "

J COLE KURUDISHA KUNDI LA TLC KWENYE 'GEMU'

RAPPER maarufu nchini Marekani J Cole yupo katika mikakati ya kuwarudisha tena kwenye ulimwengu wa muziki wadada wanaounda kundi la TLC.

Hali hiyo imetokana na baada ya kundi hilo kupotea kwenye gemu la muziki pamoja na kushindwa  kuachia albamu yao mpya  kwa muda mrefu, hali inayochagia mashabiki wao kuwasahau.

J Cole ameweka mikakati ya kurudisha kundi hilo ambapo teyari amesharekodi nyimbo aliyoshirikiana na kundi hilo inayojulikana kwa jina la 'Crooked Smile', ambapo amekiri kuwa wadada hao wamefanya vizuri kwenye nyimbo hiyo.


Monday, September 23, 2013

HALI TETE KUOKOA MATEKA JENGO LA WESTGATE KENYA

HUKU  hali ya mshikemshike ikiendelea kushuhudiwa katika jengo la Westgate lenye maduka, ufyatulianaji risasi umesikika ndani ya jengo hilo lenye maduka na migahawa zaidi ya themanini.

Wapiganaji wa Al shabaab wamewateka nyara raia ambao idadi yao haijulikani bado, waliokuwemo ndani ya jengo wakiendelea na shughuli zao kuanzia Jumamosi mchana wakati wapiganaji wa Al shabaab walipowavamia na kuanza kufyatua risasi kiholela.

Inaarifiwa kuwa  kuna miili ya watu kumi waliopoteza maisha katika ghorofa ya kwanza ya jengo hilo, aidha wapiganaji hao wanaoaminika kuwa wanachama wa Al Shabaab ni kati ya kumi na kumi na watano na bado wapo ndani ya jengo hilo.

Ripoti zinasema kuwa ufyatulianaji mkubwa wa risasi pamoja na milipuko imesikika katika jengo hilo kwa takriban dakika 15.

Harakati za kuendelea kumaliza operesheni hiyo zinaendelea lakini hali ya mateka walio ndani ya jengo hilo inaendelea kudorora. Wapo baadhi ya wakenya  waliofanikiwa kuondoka katika jengo la Westgate kwa usaidizi wa polisi.

Rais Kenyatta amesema kuwa jeshi linajitahidi kuhakikisha kuwa linakabiliana vilivyo na wanamgambo hao.

Helikopta za polisi zinazunguka juu ya jengo hilo pamoja na ndege za kijeshi kushika doria. Vikosi vya usalama vinaendelea na operesheni kujaribu kuwanusuru waathiriwa wakati hali ikiwa ikiendelea kuwa tete katika eneo la shambulizi.


Saturday, September 21, 2013

MSHINDI WA KIGOLI KUIBUKA NA GARI LA THAMANI YA MILIONI 8 NA LAKI 5

 Mashindano ya kumtafuta Kigoli wa Tanzania yapamba moto huku mshindi kuwa na uwakika wa kuondoka na gari lenye thamani ya sh milioni 8 na laki 5, huku washindi wengine wawili kupata ajira kwenye kampuni ya Chicago General Traders

Picha ikimuonesha Mratibu wa shindano la Kigoli Maimatha wa Jesse akipokea ufungua wa gari kutoka kwa Mkurugenzi wa kampuni ya Chicago Bw. Salim Chicago (kama linavyoonekana pichani), ambapo kampuni hiyo imedhamini pia mashindano hayo huku nusu fainali zikitarajiwa kufanyika 29 mwezi huyu huku washiriki 8 watakao patikana ndio wataingia kambini




Friday, September 20, 2013

HAKIMU ACHOMWA KISU

Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo iliyopo eneo la Nguzo Nane, Kata ya Kambarage Mjini Shinyanga, Satto Nyangoha amejeruhiwa kwa kuchomwa kisu katika shavu lake la kushoto baada ya kutoa hukumu ya kesi ya wizi wa baiskeli.

Kitendo hicho kinadaiwa kufanywa na mlalamikaji katika kesi hiyo, Emmanuel Izengo (28), mkazi wa Tambukareli, Shinyanga baada ya kutokuridhishwa na hukumu iliyotolewa bila ya mshtakiwa, Daniel Makelezia, mkazi wa Lubaga Shinyanga na mdhamini wake, Marko Nkelezia kuwepo mahakamani.

Katika hukumu yake, Hakimu Nyangoha alisema mshtakiwa atakapopatikana atatumikia kifungo cha miaka miwili jela baada ya kupatikana na hatia ya wizi wa baiskeli hiyo aina ya Neria yenye thamani ya Sh150,000.

Awali, ilielezwa kwamba baada ya tukio hilo la wizi lililotokea Agosti Mosi, mwaka huu katika eneo la Nguzo Nane, mshtakiwa alikamatwa na kuwekwa mahabusu na kufunguliwa kesi namba 460 ya 2013 kabla ya kuachiwa kwa dhamana Agosti 23, mwaka huu huku kesi yake ikiendelea na pande zote mbili zilitoa maelezo.


IDD AZZAN ATOA ONYO KWA WAHITIMU DARASA LA SABA


MBUNGE wa Jimbo la Kinondoni Idd Azzan amewataka wanafunzi waliomaliza elimu ya darasa la saba wasijidumbukize katika makundi ya madawa ya kulevya na badala yake waendelee na masomo ili wapate mafanikio hapo baadaye.

Hayo alisema juzi katika mahafali ya pili ya darasa la saba katika shule ya msingi ya hekima iliyopo Tandale jijini Dar es Salaam.

Alisema kuna ushawishi mkubwa wa wanafunzi wanaomaliza darasa la saba kuingia katika vishawishi vya uvutaji wa madawa ya kulevya kwa sababu wanamuda mrefu wanakuwa nyumbani hivyo hujifunza vitu mbalimbali ambavyo vingine ni kujiingiza katika makundi yasiyofaa.

Hivyo aliwataka wazazi na walezi wawapeleke watoto wao shule hata kama hajabahatika kuchaguliwa kujiunga  kidato cha kwanza.

Vile vile, aliwataka wazazi hao wawapeleke  watoto wao pre form one huku wakiwa wanasubili majibu yao kutoka na si kumuacha nyumbani na kumsababishia kujiunga katika makundi maovu.

Pia katika mahafali hayo mwalimu mkuu wa  shule hiyo Munga Mtengeti alimwambia Mbunge huyo kuwa shule yao inaupungufu wa madawati 363 na vyumba vya madarasa 3 na hawana uzio katika shule hiyo hali inayosababisha kupata kero nyingi kutoka katika nyumba zilizokuwa karibu na shule hiyo.

Hata hivyo Mbunge huyo ameahidi kutoa madawati 100,ma kujenga chumba kimoja cha darasa na amewataka wazazi na walezi wa shule hiyo kujichangisha wenyewe kwa wenyewe kwa ajili  ya kujenga vyumba viwili vya madarasa.

Katika suala la uzio wa shule Azzan amewata uongozi mzima wa shule wakishrikiana na wazazi waanze kujenga uzio huo na watakapofikia yeye atamalizia ili kuondoa kero wanazopata wanafunzi hivi sasa.



SITTA AJIONEA UZALISHAJI KIWANDA CHA BIA SERENGETI


Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki Samuel Sitta akisikiliza maelezo kutoka kwa Packaging Manager wa kiwanda cha bia cha Serengeti (SBL) kilichopo jijini Dar es Salaam, wakati alipotembelea kiwanda hicho kujionea uzalishaji unaofanya pamoja na changamoto zinazozikumba kiwanda hicho.



Wednesday, September 18, 2013

KIATU KIREFU CHAMUUMBUA JAYDEE

MSANII nyota wa muziki wa kizazi kipya nchini, Judith Wambura 'Lady Jaydee' a.k.a Annaconda, amejikuta katika wakati mgumu baada ya kiatu kirefu alichokivaa, kutaka kumwangusha jukwaani alipokuwa anatumbuiza kwenye tamasha la hitimisho la Kili Music Tour.

Tukio hilo la kutaka kuanguka lilitokea mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam katika viwanja vya Leaders Club, Kinondoni lilipofanyika tamasha hilo huku kiatu hicho kuonekana ndiyo chanzo cha msanii huyo kutaka kuanguka.

Msanii huyo alipanda jukwaani hapo akiwa amevaa 'High heels' kama kawaida ya shoo zake, lakini siku hiyo kiatu hicho kilionekana kutaka kumuumbua.


KESI DAWA ZA KULEVYA YACHANGANYA MAWAKILI

Kesi ya dawa za kulevya inayomkabili raia wa Kenya, Mwanaidi Ramadhani Mfundo, maarufu kwa jina la Mama Leila au Naima Mohammed Nyakiniwa na wenzake wanane, imeendelea kugubikwa na utata wa kisheria na kuzua mvutano uliosababisha iahirishwe kwa mara nyingine ili kusubiri uamuzi wa Mahakama.

Jana, Mahakama Kuu ilitengua hoja iliyozua mvutano mkubwa juzi kwa kuruhusu upande wa mashtaka kuwasilisha notisi ya kuongeza shahidi muhimu kutoka Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Eva Mamuya jambo lililopingwa na upande wa utetezi. Mbali ya Mama Leila, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Anthony Arthur Karanja na Ben Ngare Macharia (wote Wakenya). Wengine ni Watanzania watano, Sarah Munuo, Almas Said, Yahya Ibrahim, Aisha Kungwi, Rajabu Juma Mzome na John William.

Wakati upande wa utetezi ukipinga uamuzi huo wa jana, upande wa mashtaka ulitoa hoja nyingine ya kuongeza shahidi wa pili, ASP Neema na kuibua mvutano mkali wa kisheria uliomlazimu Jaji Grace Mwakipesile anayesikiliza kesi hiyo, kuiahirisha hadi Ijumaa wiki hii atakapotoa uamuzi kama upande wa mashtaka ulikuwa sahihi au la kuwasilisha notisi hiyo mahakamani kabla ya uamuzi wa jana.


MABANDA YA VIDEO KICHOCHEO UBAKAJI

IMEBAINIKA kuwa uwepo wa mabanda ya kuoneshea video mitaani ambayo hayapo kisheria, kumechangia vitendo vya ubakaji na ulawiti wa watoto wadogo ambao ni wanafunzi wa shule za msingi wilayani Kibaha mkoani Pwani.

Kwa mujibu wa uchunguzi uliofanywa na mwandishi wa habari hii mjini Kibaha, umebaini kuwa watoto hao wamekuwa wakifanyiwa vitendo hivyo nyakati za usiku, wanapokuwa wamekwenda kuangalia video ambapo waoneshaji wa video hizo huonesha picha chafu za ngono.

Mabanda hayo ambayo mengi yamejengwa kwa mbao au mifuko ya sandarusi na kuezekwa na makuti au nyasi na yasiyo na mvuto yamekuwa yakionesha picha hizo maarufu kama pilau, kachumbari na ubwabwa na majina mengine ambayo kwa mtu wa kawaida si rahisi kujua maana yake.


Monday, September 16, 2013

WALIMU WAANZA MGOMO UGANDA

Walimu wa shule za msingi na sekondari nchini Uganda wamegoma hii leo ikiwa siku ya kwanza ya muhula wa tatu na wa mwisho mwaka huu kwa wanafumzi.
Hii ni baada ya matakwa yao ya kutaka wizara ya elimu kuwalipa mshahara zaidi kugonga mwamba.

Walimu hao wanataka nyongeza ya asilimia ishirini pamoja na kuitaka serikali kuboresha mazingira ya kazi.
Mwalimu wa shule nchini Uganda hulipwa dola 98 kwa mwezi wakati mwalimu wa sekondari anapokea dola 176 kila mwezi.

Duru zinasema kuwa walimu waliamua kuwa watafika madarasnai ingawa hawatawafundisha wanafunzi. Hii ni kutokana na madai kuwa serikali inawatisha kuwafuta kazi walimu watakaoshiriki mgomo huo.


YANGA YAWASILISHA RUFAA YAKE

Klabu ya Yanga tayari imewasilisha rufaa yake kwa shirikisho la soka nchini TFF juu ya kucheza mchezo wake katika hali isiyokuwa na usalama na kuomba mchezo huo urudiwe katika uwanja wa ugenini kwa timu zote.

Mchezo hu ambao ulitawaliwa na vurugu kutoka kwa washabiki wa Mbeya City ulichezeshwa na mwamuzi Andrew Shamba kutoka mkoani Pwani ambaye pia hakutoka maamuzi sahihi kwa kukataa bao halali la mshambuliaji Didier Kavumbagu dakika ya 70 ya mchezo.


Mashabiki wa Mbeya City walirusha chupa za bia na mawe kwenye bus la timu ya Yanga na kuvunja kioo cha bus kubwa upande wa dereva na kumjeruhi mkononi hali iliyoplekea wachezaji wa Yanga kucheza kwa hofu katika mchezo huo wakihofia usalama wao.


Afisa habari wa Yanga Baraka Kizuguto aliwasilisha taarifa hizo kwa kamisaa wa mchezo juu ya matukio hayo na ushahidi wa kipande cha chupa kilichorushwa na kumjeruhi dereva baada ya kupasua kioo.


Tukio hilo la kabla ya mchezo lilipelekea timu ya Yanga kucheza kwa woga na wasiwasi juu ya usalama wao(under protest) kitu ambacho kikanuni kinairuhusu timu iliyokutwa na matatizo hayo kuka rufaa kuhusiana na hali ya usalama iliyojitokeza.


Aidha klabu ya Yanga pia inaomba kuhakikishwa usalama na shirikisho la soka nchini (TFF) katka mchezo wa siku ya jumatano dhidi ya timu ya Prisons vinginevyo inaomba mchezo huo pia uhamishiwe katika uwanja wa ugenini kutokana na kutokua na uhakika wa usalama.

Katika mchezo huo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania bara ulimalizika kwa sare ya bao 1-1, mchezo uliofanyika katika dimba la uwanja wa kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya.

Friday, September 13, 2013

'CHANGUDOA' , OMBAOMBA WAKAMATWA

Ombaomba zaidi ya 200 na wasichana wanaofanya biashara ya ngono maarufu kama ‘dada poa’  usiku wa kuamkia jana walikamatwa kwenye operesheni maalumu ya kuwaondoa katika maeneo mbalimbali ya jiji,iliyofanywa kwa ushirikiano wa Polisi na askari wa jiji.

Ombaomba na kinadada hao walikamatwa kwenye Manispaa ya Kinondoni na Ilala ambapo baadaye walihifadhiwa kwenye Viwanja vya Maonyesho ya Biashara ya Kimataifa(Sabasaba) kabla ya kufikishwa kwenye Mahakama ya Jiji kwa makosa ya uzurulaji.

Ombaomba hao baada ya kufikishwa mahakamani hapo  walitakiwa kurudi katika makazi yao kuanzia leo  ili wasichukuliwe hatua za kisheria.


SUALA LA MAPADRI KUOA LAJADILIWA VARTICAN

Suala la mapadri wa Kanisa Katoliki kuoa au la, limeibuka upya na tayari limeanza kuzua mijadala mikali duniani. Mjadala wa sasa umeibuliwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Vatican, Askofu Mkuu Pietro Parolin ambaye aliteuliwa hivi karibuni kushika wadhifa huo aliposema useja, yaani maisha ya utumishi ndani ya kanisa bila ndoa siyo imani, bali utamaduni na mazoea.

Akizungumzia kauli hiyo, Msemaji wa Vatican, Federico Lombardi alisema kauli ya Askofu Parolin haipingani na mafundisho ya kanisa.

Askofu Mkuu Parolin ambaye aliteuliwa karibuni na Papa Francis kushika wadhifa huo kutoka kwa Kardinali Tarcisio Bertone amenukuliwa na Gazeti la El Universal la Venezuela, Amerika ya Kati akieleza kuwa suala hilo linaweza kujadiliwa.


UN YAISHANGAA TANZANIA KUWAFUKUZA WAKIMBIZI

Umoja wa Mataifa umesema kuwa takriban wakimbizi elfu 25 kutoka Burundi wameondoshwa Tanzania kwa nguvu katika mwezi mmoja uliopita.

Afisa wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia wakimbizi UNHCR amesema malori yanayowasafirisha warundi yamekuwa yakivuka mpaka kila siku , huku wahamiaji haramu wengi wakikosa mahitaji muhimu kama vile maji na chakula

Katika wiki za hivi karibuni, Tanzania imekuwa ikiwarejesha makwao kwa nguvu wale walioelezwa wahamiaji haramu kutoka Burundi, Rwanda na Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Congo.



Wednesday, September 11, 2013

WANAWAKE ZAIDI YA 26 WAPOTEZA MAISHA KILA SIKU

TWAKIMU za hivi karibuni zinaonesha kuwa Tanzania ni kati ya nchi zinazoongoza kwa idadi kubwa ya vifo votokanavyo na uzazi huku wanawake 26 hupoteza maisha kila siku ambapo vifo hivyo asilimia 19 vinachangiwa na utoaji wa mimba usio salama.

Takwimu hizo ziimetolewa na shirika lisilo la kiserikali Marie Stopes (MST) ambapo iliweka wazi kuwa asilimia 16 tu ya vijana ndio walio katika umri wa uzazi wanatumia njia za kisasa za uzazi wa mpango


Tuesday, September 10, 2013

MWANAUME KUFUNGA NDOA NA MBUZI

Mwanaume mmoja nchini Brazil anatarajia kufunga ndoa na mbuzi wake ingawa aliahidi kutoikamilisha ndoa hiyo kwa ngono. Bw. Aparecido Castaldo, (74) anatarajia kuoana na kipenzi wake mbuzi aitwaye Camelita ifikapo Oktoba 13 mwaka huu, baada ya kuamua kutaka kumaliza siku zake za kuishi akiwa na mbuzi wake.

Kwa mujibu wa gazeti la Red Pepper la nchini Uganda, habari hiyo ambayo watu wengi wameiita ya mzaha inaripotiwa kuamsha hasira katika mji wa Jundiai jimbo la Sao Paulo anakoishi Castaldo.

Mwanaume huyo amekuwa katika mapenzi na mbuzi huyo kwa miaka miwili sasa na amesema mbuzi huyo anafaida nyingi zinazotokana na mwenza wake binadamu.

Thursday, September 05, 2013

AUNT EZEKIEL KUKATWA MKONO

MSANII wa filamu za bongo , Grayson Gwantwa Aunt Ezekiel yupo hatarini kukatwa mkono kutokana na
jeraha la kupigwa chupa lililotokea Agosti 26 mwaka huu Dar es SalaamTukio la Aunt kupigwa chupa na mwanamke aliyetajwa kwa jina moja la Yvonne nje ya Club Bilicanas, Posta jijini Dar, lilitokea  wakati staa huyo alipokwenda kujiachia na mshosti zake.


BUNGE LAGEUKA UWANJA WA NGUMI LEO

UKUMBI wa Bunge leo uligeuka kuwa ulingo wa ngumi baada ya wabunge wa kambi ya upinzani kutunishiana  misuri na askari wa bunge hilo ambapo  Kiongozi mkuu wa kambi ya upinzani Freeman Mbowe alipoamliwa kutoka nje na Naibu Spika Job Ndugai.

Hatua hiyo ilitokana  baada ya wabunge hao kupiga kura za kukubali au kukataa kuhusu kupitishwa kwa kujadili Mswaada wa Katiba uliopelekwa Bungeni hapo na Serikali ili kuweza kujadiliwa na bunge hilo.

Wabunge hao wa kambi ya upinzani wakiongozwa na Freeman Mbowe walipinga matokeo hayo na kuamua kusimama na wakati huo huo Spika Ndugai aliwataka kukaa chini ili kuendelea na kuchangia hoja za msingi za kujadili mswaada huo.

Ndugai aliwataka wabunge hao kukubaliana na matokeo yaliyotokea na kwa pamoja waweze kujadili mswaada huo ambao ni faida kwa taifa lakini mbali na ombi hilo kambi ya upinzani walikaidi ndipo Spika alitoa dakika tano kwa za kiongozi huyo kutoka ili bunge liendelee,ambapo hata hivyo kiongozi huyo alikaidi amri hiyo.


Wednesday, September 04, 2013

MAHAKAMA YASITISHA KUFUKUZWA KWA WANAFUNZI WAJAWAZITO


Hukumu ya hivi karibuni ya mahakama ya kikatiba imethibitisha kwamba shule haziwezi kuwafukuza wanafunzi kwa kupata uja uzito.Lakini Afrika Kusini bado inang'ang'ana kukabliana na suala hilo linalowaathiri wasichana 180,000 kila mwaka.

Daktari Jay-Anne Devjee ambaye ni mkuu wa afya ya akina mama katika hospitali ya King Dinuzulu anasema kwa mara nyingi hulazimika kuwazalisha wasichana kwa njia ya upasuaji, jambo linaloongeza hatari ya kuvuja damu na kuhatarisha maisha ya wazazi hao.

Phumla Tshabalala, mwenye umri wa miaka 16, anamshikilia mwanawe mchanga aliye na umri wa siku moja.Hii ni mara yake ya kwanza kujifungua na anasema ana wasiwasi kuhusu uwezekano wa kumlea mwanawe peke yake.Msichana mwenye umri mdogo zaidi hapa ana umri wa miaka 14 na anaonekana kuzidiwa na uchungu wa uzazi kiasi cha hata kushindwa kuongea.


FEDHA YAMJERUHI MWANAMKE

Mwanamke wa kimarekani amelazwa hospitali baada ya kuumia kooni na tumboni wakati akijaribu kutoa kiasi kikubwa cha fedha alizozimeza kwa kutumia ufagio wa kusafisha choo.

Christie Black 43 mkazi wa Bulls Gap, katika jimbo la Tennessee, alipata majeraha hayo baada ya kushindwa kutoa dola za Marekani 5000 alizomuibia mpenzi wake ambaye ni Bobby Gulley.

Kwa mujibu wa taalifa ya polisi wa jimbo hilo, Christie, alichukua maamuzi hayo ili kukwepa kugawana fedha hizo na mpenzi wake huyo baada ya kutengana.

Taarifa hiyo iliweka wazi kuwa mara baada ya kujiingiza fagio hilo tumboni kupitia mdomoni, mwanamke huyo alisikia maumivu makali kutokana na michubuko iliyomfanya atokwe na damu mfululizo.

Hali ya mwanamke huyo inaendelea vizuri baada ya kuwahishwa hospitali alikopewa matibabu kwa haraka.

Taarifa hiyo ya polisi iliweka bayana kuwa walipata taarifa ya tukio hilo kutokana na mpenzi wake huyo aliyekwenda kushitaki kuibiwa fedha hizo na kwamba baada ya upelelezi ndipo walipombaini mwanamke huyo akiwa taabani.

Alipohojiwa mwanamke huyo juu ya uamuzi wa kumeza kiasi kikubwa cha fedha alisema alikuwa anataka zikamsaidia kujiendeleza kimaisha baada ya kupata taalifa kuwa mpenzi wake anapanga kumuacha.



Tuesday, September 03, 2013

MWANAUME ADHANIWA KUAMBUKIZA VVU

MWANAMUME Richard Thomas ambaye amefungwa gerezani kwa kumbaka mwanamke anasubiri matokeo ya vipimo vyake kama ameambikizwa virusi vya Ukimwi kutoka kwa mwanamke huyo.

Bw. Thomas alihukumiwa kifungo cha miaka mitano na miezi minne gerezani baada ya kukiri kumbaka mwanamke huyo nyumbani kwake mjini Leigh, Greater Manchester.

Mbakaji huyo alifahamu kuwa mwanamke huyo ni mgonjwa lakini hakuweza kujua kama mhanga wake ana VVU na alizimia wakati polisi walipomjulisha, Mahakama ya Liverpool Crown ilizikiliza.

Kwa mujibu wa BBC, Bw. Thomas, 27, kutoka mtaa wa Sandringham Drive, Leigh, alimbaka mwanamke huyo wakati alipokuwa amekunywa kidonge cha usingizi.


MWANAMKE AMEZA SIMU

WIVU wa kimapenzi umemuweka matatani msichana anayeishi nchini Brazil, Adriana Andrade baada ya kuamua kumeza simu yake ya mkononi ili kumzuia mpenzi wake asisome 'message' katika simu yake.

Msichana huyo mwenye umri wa miaka 19 amejikuta akilazimika kuumeza simu hiyo baada ya kugundua alikuwa na message za ajabu ambazo zingezua utata pindi mpenzi wake angezisoma.


MOHAMMED ENTERPRISES YASHINDA KESI DHIDI YA BAKHRESA

Kundi la makampuni ya MeTL imeshinda kesi dhidi ya matumizi ya haki miliki zake dhidi ya makampuni ya Bakhressa. Bakresa sasa itatakiwa kuilipa METL Group kiasi cha shilingi milioni 732 pamoja na riba.

taarifa hiyo iliwekwa hatharani katika mtandao wa Twitter na mmiliki na Mkurugenzi wa makampuni ya Mohammed Enterprises (MeTL), Mohammed Dewji MO (pichani chini) muda si mrefu kama msisitizo wa Twitt nyingine iliyowekwa na kampnuni hiyo jana.




BREAKING NEWS: MICROSOFT YAINUNUA NOKIA

Kampuni ya Microsoft imeingia makubaliano ya kununua kampuni ya simu za mkononi ya Nokia kwa kiasi cha shilingi trilioni 11.5 (uro bilioni 5.4 au dola bilioni 7.2).

Nokia pia itatoa leseni zake za hati miliki pamoja na ramani za huduma zake kwa kampuni ya Bill Gates ya Microsoft.
Kwa mujibu wa mitandao mbali mbali duniani ikiwa ni pamoja na BBC, Sky News, CNN, USA Today, Makampuni hayo kwa pamoja yalinukuliwa mbele ya waandishi wa habari kuwa makubaliano hayo yatakamilika mwanzo ni mwa mwaka 2014, wakati ambao kiasi cha wafanyakazi 32,000 wa Nokia watahamishiwa kwenye kampuni ya Microsoft.


Monday, September 02, 2013

MSHINDI MISS REDD'S PHOTOGENTICS 2013 APATIKANA


 Mshindi wa Miss Redd's Photogentics (katikati) akiwa amepozi na washiriki waliofanikiwa kuingia tano bora ya miss Photogenitics. Kinyanganyiro hicho kilifanyika juzi katika hoteli ya Giraff Dar es Salaam.



MAXMALIPO WAWAFIKIA WATEJA DAR ES SALAAM

 Ofisa Uhusiano na Masoko wa Maxmalipo Bw. Isaac Nyimbo akimpa maelekezo mteja baada ya kutembelea banda lao katika viwanja vya Posta Dar es Salaam jana.  Wakati wa tamasha la 'Elimu exprience'

 Ofisa Uhusiano na Masoko wa Maxmalipo Bw. Isaac Nyimbo akiwa na baadhi ya wafanyakazi wenzie akitoa maelekezo kwa mteja baada ya kutembelea banda lao katika viwanja vya Posta Dar es Salaam jana.  Wakati wa tamasha la 'Elimu exprience'



Sunday, September 01, 2013

WEMA SEPETU AMLIZA MAMA KANUMBA


BAADA ya mama Kanumba Bi. Flora Mtegoa kutunzwa kitita cha sh. laki tano na msanii wa filamu nchini Wema Sepetu, kitendo hicho kilimtoa machozi mama huyo na kudai kuwa kila anapokutana na baadhi ya wasanii anajikuta kumkumbuka mtoto wake.

Kitendo hiko kilitokea mwishoni mwa wiki katika uzinduzi wa Filamu ya Elizabeth Michael iliyopewa jina la Foolish Age katika ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam, ambapo mama Kanumba alijikuta akitokwa na machozi mfululizo mara baada ya kukutana na msanii huyo.

Mama huyo ambaye alijikuta akivutiwa na uchezaji wa Wema ukumbini hapo wakati bendi ya Machozi ikitumbuiza aliamua kumfuata na kutaka kumtunza kutokana na uchezaji wake.

Wema alishindwa kupokea hela hiyo aliyotunzwa na mama huyo na badala yake alianza kumtunza yeye hela hali ambayo ilimtoa machozi.

Wema alimpigia magoti mama huyo kwa ishara ya kuonyesha kuwa anamuheshimu, na kumpenda huku akizingatia alishawahi kuwa mama mkwe wake.

Akizungumza mara baada ya kutunza kitita cha fedha hizo mama huyo aliweka wazi kuwa kila anapokutana na wasanii ambao walikuwa wanaukalibi na mtoto wake huyo anajikuta anamkumbuka mwanaye.