Monday, September 16, 2013

WALIMU WAANZA MGOMO UGANDA

Walimu wa shule za msingi na sekondari nchini Uganda wamegoma hii leo ikiwa siku ya kwanza ya muhula wa tatu na wa mwisho mwaka huu kwa wanafumzi.
Hii ni baada ya matakwa yao ya kutaka wizara ya elimu kuwalipa mshahara zaidi kugonga mwamba.

Walimu hao wanataka nyongeza ya asilimia ishirini pamoja na kuitaka serikali kuboresha mazingira ya kazi.
Mwalimu wa shule nchini Uganda hulipwa dola 98 kwa mwezi wakati mwalimu wa sekondari anapokea dola 176 kila mwezi.

Duru zinasema kuwa walimu waliamua kuwa watafika madarasnai ingawa hawatawafundisha wanafunzi. Hii ni kutokana na madai kuwa serikali inawatisha kuwafuta kazi walimu watakaoshiriki mgomo huo.


Walimu hao inasemekana walitoa onyo la siku 90 kwa serikali lakini kwa sababu wanahisi kuwa serikali iliwapuuza ndio maana wakaamua kugoma.

Serikali kwa muda mrefu imekuwa ikiahidi kuwaongeza mishahara walimu hao ambao ni baadhi ya wafanyakazi wa umma wanaopokea mishahara duni katika taifa hilo la Afrika Mashariki.

Changamoto kwa Uganda imekuwa gharama ya matumizi serikalini hasa tangu wahisani kusitisha msaada kwa taifa hilo kutokana na utumizi mbaya wa pesa za umma na ufisadi.

Maafisa wa chama cha walimu wamesema kuwa takriban walimu 159,000 hawatafunza kuanzia leo hadi serikali itakapotimiza matakwa yao.

Kumekuwa madai ya maafisa wa usalama kuwatisha walimu wanaogoma , ingawa serikali imeyakanusha madai hayo.

No comments:

Post a Comment