Wednesday, September 18, 2013

MABANDA YA VIDEO KICHOCHEO UBAKAJI

IMEBAINIKA kuwa uwepo wa mabanda ya kuoneshea video mitaani ambayo hayapo kisheria, kumechangia vitendo vya ubakaji na ulawiti wa watoto wadogo ambao ni wanafunzi wa shule za msingi wilayani Kibaha mkoani Pwani.

Kwa mujibu wa uchunguzi uliofanywa na mwandishi wa habari hii mjini Kibaha, umebaini kuwa watoto hao wamekuwa wakifanyiwa vitendo hivyo nyakati za usiku, wanapokuwa wamekwenda kuangalia video ambapo waoneshaji wa video hizo huonesha picha chafu za ngono.

Mabanda hayo ambayo mengi yamejengwa kwa mbao au mifuko ya sandarusi na kuezekwa na makuti au nyasi na yasiyo na mvuto yamekuwa yakionesha picha hizo maarufu kama pilau, kachumbari na ubwabwa na majina mengine ambayo kwa mtu wa kawaida si rahisi kujua maana yake.


Baadhi ya wakazi ambao wamelaani mabanda hayo, ambayo huanza kuonesha video majira ya asubuhi hadi usiku na kusababisha baadhi ya wanafunzi kushinda humo, huku wakiwa wameaga wanakwenda shule na kuishia mabandani na endapo wazazi hawatafuatilia kuna hatari ya wanafunzi kutohudhuria darasani kabisa.

Walilielezea njia wanazotumia wabakaji hao ni kuwalipia kiingilio cha kuangalia picha ambacho ni sh. 500 kwa filamu zitakazooneshwa kwa siku hiyo, ambazo huoneshwa kwa awamu na huchukua kila awamu zaidi ya saa tatu, kisha kubadili picha zingine.

Picha zinapokuwa zinaendelea mara hubadili na kuweka picha chafu za ngono, hivyo kuhamasisha vitendo hivyo na kwa kuwa vijana hao wanaobaka watoto wanakuwa wamewalipia kiingilio, huwachukua na kuwapakata watoto hao na wanapokuwa wamepandwa na msisimko huanza kuwaingilia watoto hao hadi wanapomaliza haja zao.

“Mara wamalizapo haja zao huwapa fedha kwa ajili ya kuwataka wasiseme kwa wazazi wao ambapo watoto hao, baadaye huzoea na kujikuta kila wakati wakienda kwenye mabanda hayo na kufanyiwa vitendo hivyo na kuzoea hali ambayo inawaathiri kisaikolojia na kufanya maendeleo yao shuleni kushuka,” alisema mmoja wa wakazi hao ambaye hakupenda kutajwa jina .

Akizungumzia hali hiyo, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Lulanzi wilayani Kibaha mkoani Pwani, Anna Bilali alisema wanafunzi wengi wameathiriwa na hali hiyo, ambapo mbali ya kwenda kwenye mabanda hayo mara wasipokwenda shule huandika kazi walizofanya wenzao, kisha kujisahishia ili kuwadanganya wazazi wao.

“Wanafunzi wa namna hii wamekuwa wakijisahishia madaftari yao, lakini sisi tunagundua kwani usahishaji wao ni tofauti na wa walimu na tunapowaambia, baadhi ya wazazi wamekuwa wakiwatetea watoto wao hali inayosababisha ugumu wa kuwadhibiti, kwani baadhi ya wanafunzi hukaa kwenye mabanda hayo hadi saa tatu usiku bila hata kuulizwa walikokuwa,” alisema mwalimu huyo.

Alisema pia baadhi yao humiliki simu, ambazo wanakwenda nazo shuleni na kuangalia picha hizo na kujikuta muda mwingi wakiutumia kwa kuangalia picha hizo kupitia simu, ambazo huwa wanazificha na inakuwa vigumu kuwagundua hadi wenzao watoe taarifa.

Aliongeza kuwa kuna watu wamekuwa wakiwaonesha picha hizo kupitia simu, kisha huwatoza kiasi kidogo cha fedha kwa ajili ya kupata huduma hiyo, hali amabayo inaendelea kuongeza kusambaa kwa vitendo viovu.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mwantumu Mahiza alisema udhibiti wa mitandao kama hiyo ya uoneshaji wa picha za ngono ni viongozi wa mtaa na vijiji kwa kuwachukulia hatua, kwani hayako kisheria hivyo hayana sababu ya kuwepo ili kuondoa tatizo hilo.

Hivi karibuni wanafunzi wanne wa Shule ya Msingi Lulanzi, walikamatwa na polisi wilayani Kibaha kwa tuhuma za kumbaka mwanafunzi mwenzao wa darasa la pili, mwenye umri wa miaka tisa na kumsababishia maumivu makali na kulazwa hospitali ya Tumbi ambapo aliruhusiwa kutoka wiki iliyopita baada ya kupata matibabu.



No comments:

Post a Comment