Serikali isiyo na soni. Imefunga tovuti ya tume ya mabadiliko ya katiba, eti lengo kuu ni kuhakikisha wananchi hawapati rejea na nyaraka mbalimbali ambazo zinaweza kusaidia uelewa na ufahamu wao. Sababu ya serikali ni kuwa, kazi ya tume imekwisha hivyo na tovuto yake haina kazi
Serikali inayoogopa wananchi wake wasiendelee kuelimika, kujielimisha na kufahamu mambo muhimu ya nchi ni serikali ya ajabu sana.
Tovuti ni maktaba za kielektroniki, tume ya katiba ya Kenya hadi leo tovuti yao ipo hewani, tume ya katiba ya Ghana hadi leo inafanya kazi, ya Afrika ya kusini hadi sasa iko hewani baada ya miaka mingi ya kutunga katiba ya taifa hilo mara baada ya Madiba kuingia madarakani.
Hapa Tanzania, serikali iloituma tume kukusanya maoni ya wananchi sasa imekasirika, kwa hiyo inayapiga vita maoni ya wananchi, inaipiga vita tume ya mabadiliko ya katiba. Serikali nyingi za kiafrika zina rekodi mbaya mno kila inapotokea matakwa yake fulani yamezuiwa na na watu fulani kwa njia halali.
Kwa chuki hizi za waziwazi dhidi ya tume na Wajumbe wa tume ya mabadiliko ya katiba, natoa wito kwa wajumbe hao kuwa makini na nyendo zao na kutojiamini sana. Ikumbukwe nchi hii watu wamewahi kung'olewa macho na wengine meno na vyombo vya dola viliishia kukamata wendawazimu na kuwapa mashtaka huku wahusika halisi waliotumwa kufanya kazi hizo za kinyama kwa maslahi tusiyoyajua wakitamba mitaani hadi leo.
Nasisitiza kuwa, ikiwa serikali ya kiafrika inafunga hadi tovuti yenye taarifa za maoni ya wananchi iliyokuwa wazi kwa umma, ni muhimu wajumbe wa tume wakajichunga sana. Mimi siiamini sana serikali hii ambayo leo inaweza kukutuma kazi na kesho asubuhi ikakugeuka na kukupiga vita wewe na kazi uliyoifanya.
Haya ni maoni na mtizamo wangu binafsi. Inatosha tu kuheshimu mawazo ya kila mtu.
No comments:
Post a Comment