Tuesday, December 17, 2013

WATU 7 WAMEKAMATWA KWA MAUAJI YA KIGOGO WA CCM

JESHI la Polisi mkoani Mwanza, linawashikilia watu saba kwa tuhuma za kuhusika na mauaji ya aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), mkoani humo na Diwani wa Kata ya Kisesa, marehemu Clement Mabina (Pichani Kulia), imeripotiwa, Mwanza.

Marehemu Mabina aliuawa kwa mawe, mapanga katika eneo la Kanyama ambako kulikuwa na mgogoro wa shamba baada ya kutokea kutoelewana na wakazi wa eneo hilo.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamanda wa Polisi mkoani humo, Kamishna Msaidizi Mwandamizi, SACP Valentino Mulowola, alisema watuhumiwa hao walikamatwa jana kwa nyakati tofauti.

“Tunaendelea kuwatafuta watuhumiwa wengine ambao wanadaiwa kuhusika na mauaji haya ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa,” alisema Kamanda Mulowola.

Katika tukio hilo, marehemu Mabina aliuawa kwa kukatwa mapanga na kupigwa mawe ambapo mwili wake ulikutwa na majeraha makubwa kichwani na kichogoni.

Kabla ya mauaji hayo, marehemu anadaiwa kumpiga risasi kwa bahati mbaya mtoto mwenye umri wa miaka 11 wakati akijihami na mashambulizi ya wananchi hao.

Kamanda Mulowola alisema marehemu alikutwa na silaha mbili aina ya short-gun na bastola moja.

Habari zilizolifikia gazeti hili kutoka ndani ya jeshi hilo, zinasema mmoja wa watuhumiwa waliokamatwa alikutwa na simu ya mkononi iliyokuwa ikitumiwa na marehemu lakini Kamanda Mulowola hakutaka kutaja jina lake wala majina ya watuhumiwa wengine.

Hivi sasa, wakazi wa Kijiji cha Kanyama wanaishi kwa hofu kubwa baada ya mauaji hayo na wengine kukimbia makazi yao wakihofia kukamatwa na polisi.





No comments:

Post a Comment