Tuesday, December 17, 2013

SOKA:OKWI AITESA SIMBA

Wanachama wa Klabu ya Simba, wamechanganyikiwa baada ya habari za Emmanuel Okwi, aliyekuwa mchezaji wao kipenzi kusajiliwa na Yanga kwa mkataba wa miaka miwili. 

Wanachama hao sasa wanalia na Mwenyekiti wao, Aden Rage ambapo wanataka kujua malipo ya Okwi, ambaye Simba ilimuuza kwa Klabu ya Etoile du Sahel ya Tunisia. 

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa tawi la Mpira Pesa Ustadhi Masoud, alisema suala la Okwi kusajiliwa Yanga linawapa wasiwasi, kwani bado kuna deni katika Klabu ya Etoile du Sahel ya nchini Tunisia. 

Ustadhi alisema kitendo kilichofanyika cha Okwi, kusajiliwa kuichezea Yanga kinaonesha wazi kuwa Simba ilishalipwa na anayejua suala hilo ni Mwenyekiti wa klabu hiyo. 

Alisema, mara baada ya kupata taarifa ya kusajiliwa kwa mchezaji huyo, alikwenda hadi Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na akakutana na Mkurugenzi wa Mashindano wa shirikisho hilo, Sad Kawemba alimwabia kuwa taratibu zote za usajili zilifanyika na hati ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC) imekamilika kuhusu mchezaji huyo. 

"Kwa suala hili inaonesha wazi kabisa fedha za mauzo ya Okwi zimeshalipwa isipokuwa kuna kitu kinafichwa, ili tuendelee kuamini kuwa bado Simba inaidai Etoile du Sahel,"alisema. 

Ustadhi aliongeza kuwa, baada ya kumalizika mechi ya Ngao ya Hisani inayotarajiwa kuchezwa Desemba 21, mwaka huu watakwenda hadi nyumbani kwa Rage na kumshinikiza ajiuzulu. 

"Baada ya Mechi ya Simba na Yanga haitajalisha kuwa tumeshinda, tumeshindwa au tumetoa sare sisi tulichoamua ni kwenda hadi nyumbani kwa Rage ambako tutaomba ajiuzulu," alisema. 

Naye mwanachama mwingine wa klabu hiyo, Mgeni Ramadhani 'Macho' alisema Mwenyekiti huyo amekuwa mzungumzaji zaidi. 

Macho alisema kitakachomaliza mgogoro huo ni Mkutano Mkuu wa klabu hiyo. 

Kwa upande wake, Haruna Nazi ambaye pia ni mwanachama wa klabu hiyo alisema wanachama wenzake hawana umoja. 

"Wanachama wenzangu nawaomba muwe watulivu, tunasubiri baada ya kumalizika mechi dhidi ya Simba na Yanga ndiyo hatma ya Rage itajulikana," alisema. 

Naye Ofisa Habari wa Yanga, Baraka Kizuguto akizungumzia suala la usajili wa Okwi, alisema wao kama klabu wamefuata taratibu zote za uhamisho wa mchezaji wa ndani na nje ya nchi, ambapo wamemsajili akiwa na Sports Villa hivyo viongozi wa Simba hawamdai Okwi bali wanaidai Etoile du Sahel


No comments:

Post a Comment