Friday, December 20, 2013

HOTELI 9 ZA KITALII ARUSHA KUFUNGWA

Hoteli tisa zenye hadhi ya kitalii jijini Arusha,huenda zikafungwa kutokana na mamlaka ya maji safi na maji taka mkoani Arusha(AUWSA)kuziba mkondo wa kutoa maji machafu ,hali iliyosababisha harufu kali na maji machafu kufurika ndani ya hoteli hizo na kuhatarisha afya za watumiaji. 

Hata hivyo tayari naibu Meya wa Jiji la Arusha, Prosper  Msofe amemwagiza Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka Arusha (AUWSA) kuhakikisha anafungua chemba za maji machafu walizozifunga kwenye hoteli tisa zilizopo Jijini hapa. 

SOMA ZAIDI...

Amesema endapo hoteli hizo hazitafunguliwa chemba za kupitisha maji machafu basi wananchi wa Jiji hilo watachukua hatua ikiwemo ya kwenda kufungua chemba hizo ili kunusuru afya za watalii na wageni mbalimbali ambao wanahitaji huduma za malazi katika hoteli hizo.

Msofe aliyasema hayo juzi jijini hapa wakati alipokuwa akiwaelezea waandishi wa habari juu ya uamuzi uliochukuliwa na AUWSA  wa kuamua kufunga chemba za maji machafu kwenye hoteli tisa za jijini hapa ambazo zinalaza wageni mbalimbali na kuhatarisha huduma za utalii,kwa madai kwamba zinaiba maji. 

Alisema mamlaka hiyo haikutumia busara kwa kufungia hoteli hizo pasipo kuwapa notisi iwapo imebaini kuwepo ukwepaji wa kulipa huduma ya maji safi ,na kusababisha shirika hilo kushindwa kujiendesha.

AUWSA ikumbuke kuwa miundombinu yake ya maji safi  si mizuri hizo hivyo kitendo cha kufunga maji na chemba za kutiririsha maji katika  hoteli hizo ni ukosefu wa hekima za utendaji kazi. 

Tunamtaka Mkurugenzi wa AUWSA,Injinia Ruth Koya kuhakikisha anarudisha maji kwenye hoteli za Naura Spring, Rich Hotel, Mid -Way, Sterio Hoteli,Hil Town, Aquline, Seven Eleven na hoteli mbili ambazo hakuzitaja. 

Hata hivyo mwandishi wa habari hii alipomtafuta Mkurugenzi wa AUWSA kwa njia ya simu ya kigangani, alisema kuwa amepokea taarifa hiyo na anaifanyia kazi. 

Aidha alisema kuwa ukosefu wa maji safi na salama kunaweza kuhatarisha afya za wananchi kwani maji hayo yanaweza kutiririshwa mitaani na kusababisha magonjwa mbalimbali kama vile kipindu pindu na magonjwa mengine. 

Hata hivyo msako huo wa kubaini wezi wa maji unaendelea katika mkoa wa Arusha ikiwa ni zoezi endelevu la kubaini wabadhilifu wanaoihujumu serikali kwani hotel hizo zinauwezo wa kulipa fedha kwa mamlaka hiyo  Mwisho.




No comments:

Post a Comment