Wednesday, February 10, 2016

KAMATI YA LAAC NA PAC ZAPEWA SOMO NA TAMISEMI

WABUNGE wametakiwa kuzisimamia halmashauri ili ziwe zinachukua hatua za kisheria za kudhibiti ujenzi holela katika miji mbalimbali nchini. Kauli hiyo ilitolewa jana na Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Sheria kutoka ofisi ya Rais,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI),Eustard Ngatale.

Ngatale alikuwa akijibu hoja za wabunge katika semina ya wabunge wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Serikali za Mitaa (LAAC) na Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC).

Alisema suala la ujenzi holela halipo Tanzania peke yake bali ni tatizo kwa dunia nzima. "Lazima halmashauri ziwe zinachukua hatua ili kudhibiti ujenzi holela katika miji,"alisema.

Awali Mwenyekiti wa Kamati ya LAAC,Kangi Lugola alihoji sababu za halmashauri nyingi kutokuwa na mipango miji wakati kila halmashauri inao maafisa mipango miji. Aidha,Lugola alitaka fedha za Mfuko wa Jimbo zitengewe akaunti yake badala ya kuchanganywa na akaunti nyingine za halmashauri.

Wajumbe hao wa Kamati ya LAAC na PAC walipewa semina kuhusu Majukumu ya TAMISEMI na Usimamizi wa Shughuli zake na Muundo na Majukumu ya Ofisi ya Rais TAMISEMI. Wajumbe hao pia walijifunza sheria mbalimbali za Serikali za Mitaa ikiwemo Sheria ya Mamlaka za Serikali za Mitaa sura 288 na Sheria na Sheria za Leseni za Vileo Sura 77.

Akizungumzia semina hiyo,Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI,George Simbachawene alisema semina hiyo itawawezesha wajumbe wa LAAC na PAC kuyajua majukumu yao hivyo wataweza kuisimamia Serikali ipasavyo.





No comments:

Post a Comment