Wednesday, February 10, 2016

BALOZI WA JAPAN AKABIDHI GARI YA HUDUMA YA DHARURA KWA MKEMIA MKUU

Na Beatrice Lyimo-Maelezo
Dae es Salaam

Balozi wa Japan nchini Tanzania Masaharu Yoshida amekabidhi Gari la huduma ya dharura (AMBULANCE) kwa Kituo cha Uratibu wa Matukio ya Sumu nchini kilichopo chini ya Wakala wa Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali.

Makabidhiano hayo yamefanyika leo jijini Dar es salaam kati ya Balozi huyo na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu sambamba na kuzindua Cheti cha Ithibati cha kuitambulisha Maabara hiyo kimataifa.

Akizungumza mara baada ya kukabidhi gari hilo Balozi Yoshiba amesema kuwa Jumuiya ya Zimamoto ya nchini Japan imetoa magari 83 kwa Tanzania ikiwemo magari 10 ya huduma ya dharura kwa nia njema na pia kukuza uhusiano wa kirafiki kati ya Tanzania na Nchi ya Japani.

Amesema Jumuiya hiyo ilianza kutoa magari hayo tangu mwaka 2006 na kuahidi kuendeleza uhusiano huo wa kirafiki wenye manufaa kati ya Tanzania na Japani.

Kwa upande wake Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu amesema kuwa makabidhiano ya gari hilo yameleta hamasa kwa upande wa Wakala na Wadau wengine katika kukabiliana na matukio ya Sumu nchini.

“Ili Taasisi iweze kufanya kazi kwa ufanisi uwepo wa miundo mbinu kama vifaa ikiwemo mitambo, vitendea kazi kama vile magari na majengo bora ni suala ambalo halina budi kupewa kipaumbele”alisema Waziri Ummy.

Pia Waziri Ummy amesema kuwa Serikali inatambua umuhimu na unyeti wa majukumu yanayotekelezwa na Wakala wa Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali katika kulinda afya, mazingira na usalama kwa watu na hivyo kuleta utengemano katika jamii.

Aidha, Waziri Ummy amezindua cheti cha Ithibati chenye namba ISO 1705:2005 kinachoitambulisha maabara ya Mkemia Mkuu kimataifa.

Katika hatua nyingine Waziri huyo ametoa agizo kwa Wakala wa maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kutoa kipaumbele suala la Madaya ya Kulevya kwa kuwapima watoto haswa wa shule za msingi na sekondari ili kuweza kupambana na janga hilo.


No comments:

Post a Comment