Wednesday, February 10, 2016

MBUNGE ATAKA ‘BOSI’ MKUU EWURA APEWE ULIZI

KATIKA hali isiyo ya kawaida, Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Bw. Yusufu Kaiza Makame (CUF-Chake Chake), amehoji kama Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), Bw. Felix Ngamlagosi (PICHANI), ana ulinzi kutokana na kazi nzito anayoifanya katika masuala ya udhibiti.

Bw. Makama alihoji jana kuhusu ulinzi kwa Bw. Ngamlagosi wakati EWURA ilipokuwa inaeleza shughuli mbalimbali kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini iliyokutana Dar es Salaam, ambapo kambla ya kuchangia masuala mbalimbali Bw. Makame aliuzia: “Hivi una mlinzi wewe?, ndipo Bw. Ngamlagosi aliposimama na kujibu “sina mlinzi Mheshimiwa,” hatua iliyowafanya wabunge kuangua kicheko.

Bw. Makame alisema EWURA imekuwa inapmbana na watu na wafanyabiashara wenye uwezo wa kifedha hali ambayo ni hatari kwa watumishi kama Bw. Ngamlagosi; maelezo yaliyofanana na wabunge wengi kuwa EWURA imekuwa ikilalamikiwa sana na wafanyabiashara na umma kwa ujumla kuwa wamekuwa wakiwanyanyasa.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Bi. Matha Mlata, akizungumzia kuhusu tuhuma za EWURA kunyanyasa wafanyabiashara, alikiri naye kupokea malalamiko ya kuwepo kwa unyanyasaji huo kwa wafanyabiashara wa mafuta na EWURA hali ambayo alisema ataifuatalia.

Hata hivyo, habari ambazo zilipatikana jana zilieleza kuwa wadau wanaolalamika ni wale ambao wamekuwa wakikamatwa na EWURA wakiuza mafuta ya kwenda nje katika soko la ndani. Habari zaidi zilisema katika kipindi cha hivi karibuni baadhi ya wafanyabiashara wameadhibiwa na EWURA adhabu kali, hivyo kuamua kula sahani moja na EWURA kwa kuisambaratisha kabisa isiwepo.

Alipoulizwa juu ya kuwepo mchakato wa kuisambaratisha EWURA, Meneja wa Mawasiliano na Uhusiano wa EWURA, Bw. Titus Kaguo; alisema amekuwa akisikia minong’ono ya aina hiyo ingawa anaamini haina ukweli wowote.

Alipoulizwa kuwepo kwa malalamiko ya EWURA kunyanyasa, Bw. Kaguo alisema kwa kuwa wamekuwa wakitoa adhabu kali kwa wanaokiuka sharia na taratibu kuna uwezekano mkubwa wafanyabishara wanoadhibiwa wakawa wanalalamika.

“Inawezekana kabisa kuwepo na malalamiko, lakini ukweli ni kwamba EWURA inafanya kazi zake kwa kufuata Sheria, Kanuni na Taratibu zilizopo ambapo mtu akikiuka; kwa mfano amekutwa akiuza mafuta ya kwenda nje katika soko la ndani adhabu yake kwa mara ya kwanza ni sh millioni 7/” alisema Bw. Kaguo na kuongeza “ Ukikutwa kwa mara ya pili unalipa Sh milioni 25 EWURA na kulipa kodi TRA kulingana na uwingi wa mafuta uliyokwepa kulipia kodi”.

Alisema adhabu kama hizo ambazo wafanyabiashara wengi wamekuwa wakikkubwa haziwezi kuwafurahisha hata kidogo.

Katika kamati hiyo, EWURA iliwasilisha taarifa ya jinsi ilivyoanzishwa, muundo, majukumu, mlingano wa bei za soko la dunia na hapa nchini, pamoja na ubora wa mafuta yanayotumika hapa nchini. Pia Kamati hiyo ilikutana kwa pamoja na Wakala wa Uagizaji wa Mafuta kwa Pamoja (PBPA), ambayo pamoja na mambo mengine, Kaimu Mtendaji Mkuu wa PBPA, Bw. Michael Mjinja alielezea kuwa Wakala wake unachangamoto ya upotevu wa mafuta yanapotoka kwenye meli kwenda kwenye maghala.




No comments:

Post a Comment