Wednesday, February 10, 2016

BARABARA YA MUGUMU SERENGETI KUKAMILIKA MWEZI MEI

Na Jacquiline Mrisho-MAELEZO

Barabara ya Mji wa Mugumu wilayani Serengeti mkoani Mara inatarajiwa kukamilika mwezi Mei baada ya kushindwa kukamilika ndani ya muda uliopangwa.

Akiongea kwa njia ya simu leo,Afisa Habari Wilaya ya Serengeti Englibert Thomas Kayombo amesema kuwa, Barabara hiyo ilitakiwa kukamilika Januari 6 lakini kutokana na changamoto mbalimbali barabara hiyo haikuweza kukamilika kwa wakati.

“Ujenzi wa barabara una hatua mbali mbali ambazo zinafanywa kabla ya hatua ya mwisho ya kuweka lami, ikiwemo uchimbaji wa mitaro na kuondoa miundo mbinu yote iliyo katika barabara”Alisema Kayombo

Amezitaja baadhi ya changamoto hizo ni kuwepo mabomba ya maji na nguzo za umeme yaliyopita katika barabara inayotarajiwa kuwekwa lami hivyo shughuli zilisimama ili kupisha zoezi la kuhamisha mabomba na nguzo hizo pia hali ya hewa, ya Mji wa Mugumu hupata mvua kubwa zinazonyesha kwa kipindi cha muda mrefu hivyo kupelekea zoezi la ujenzi wa barabara kwenda kwa taratibu.

Ameongeza kuwa,kutokana na changamoto hizo ujenzi wa barabara ya lami katika Mji wa Mugumu Serengeti ulisimama kwa muda hivyo mkandarasi ameongezewa muda hadi mwezi Mei 2016 ili kukamilisha ujenzi wa barabara hiyo.

Katika mwaka wa fedha 2014/15 Serikali ilitenga bajeti ya ujenzi wa barabara ya Mji wa Mugumu yenye kilomita 3 kwa kiwango cha lami na kazi hiyo iko chini ya Kampuni ya SAMOTA Ltd.

No comments:

Post a Comment