Na Beatrice Lyimo- MAELEZO, Dar es Salaam
Kijana Joseph Stanford kutoka Mabatini wilaya ya Nyamagana jijini Mwanza amempongeza Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli kwa utendaji wake wa kazi ambapo ametembea kutoka Mwanza hadi Dar es salaam kwa muda wa siku 25.
Kijana huyo alianza safari yake jijini Mwanza Januari, 16 mwaka 2016 saa 10:00 alfajiri na ambapo safari hiyo ameihitimisha jijini Dar es salaam Februari 9, 2016 jioni.
“Matembezi yangu ni ya hiari na lengo la kutembea huku ni kumpongeza na kumuunga mkono Rais Magufuli juu ya utendaji wake wa kazi anaoufanya na pia kumshukuru kwa kuunda Wizara ya Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo” aliongeza Joseph.
Hata hivyo, kijana Joseph alisema kuwa katika matembezi yake alikumbana na changamoto nyingi ikiwemo ukosefu wa wadhamini katika kufanikisha safari yake ya kumpongeza Rais Magufuli.
Kwa upande wake Wizira wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Nape Nnauye amesema kuwa anatambua uwepo wa kijana huyo na amempongeza kwa hatua hiyo ya kishujaa aliyoionesha.
Mbali na hayo, Kijana huyo ameomba kuwezeshwa kukutana na Rais mstaafu Jakaya Kikwete ili kumshukuru kwa kuthamini na kuibua vipaji vya vijana nchini. Joseph anaumri wa miaka 20 na pia ni muhitimu wa kidato cha nne mwaka 2015 katika shule ya Sekondari Mtoni iliyopo jijini Mwanza.
No comments:
Post a Comment