Thursday, June 21, 2012

TANROADS WASITISHA AJIRA


Na mwandishi wetu, Kilimanjaro

WAKALA wa Barabara nchini (TANROADS) Mkoa wa Kilimanjaro imesitisha ajira kwa watumishi wanne wa Mizani ya Himo Njiapanda katika kipindi cha kuanzia Januari 2011 hadi April 2012, baada ya kuonekana kuwa sio waadilifu.

Hayo yalibainjishwa na Meneja wa wakala huyo mkoani humo Bw. Rubirya Marwa wakati wa kikao cha Bodi ya Barabara ambapo alisema kumekuwepo na baadhi ya watumishi wasiowaaminifu hali ambayo imekuwa ikizorotesha utendaji kazi.

Alisema, baadhi ya watumishi wa mizani hushawishiwa na wasafirishaji ili waachie magari yaliyozidisha uzito hivyo kujikuta wakijiingiza kwenye vitendo vya rushwa jambo ambalo ni kinyume cha sheria.

Aidha, alisema ofisi yake itaendelea kuwaondoa wafanyakazi ambao watakiuka maadili ya kazi na pale ambapo ushahidi utapatikana hawatasita kuwafikisha katika vyombo husika ili kuwa fundisho kwa watumishi wengine wenye tabia kama hizo.

Kutokana na hali hiyo Mhandisi Rubirya aliwataka wasafirishaji kuwafichua wafanyakazi wanaodai rushwa ili uongozi na vyombo vingine vya dola ikiwemo Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) viwachukulie hatua stahili.

Alisema, katika kipindi hicho jumla ya magari 136,176 yalipimwa uzito katika mizani hiyo na kati ya hayo magari 17,694 yalionekana kuzidisha uzito wa kilo 9,079,966 ambapo jumla ya sh. mil.191.021 zilikusanywa katika kipindi hicho.

Alisema shilingi mil.188.621 zilitokana na magari 2,638 yaliyotozwa gharama za uharibifu na sh. milioni 2.40 zilitokana na adhabu mbalimbali ambazo ni pamoja na kukwepa mizani.

Alisema, pamoja na jitihada hizo bado wanakabiliwa na changamoto mbalimbali katika mizani hiyo ikiwa ni pamoja na vishawishi vya rushwa na ukiukwaji wa sheria kwa makusudi.

Alisema, changamoto nyingine ni baadhi ya wasafirishaji kutumia lugha chafu na vitisho kwa wafanyakazi wa mizani hali ambayo imekuwa ikiathiri utendaji kazi na kusababisha foleni kubwa.



No comments:

Post a Comment