Wednesday, June 13, 2012

WATUMISHI KIZIMBANI KWA UBADHIRIFU


Na waandishi wetu

WATUMISHI wawili wa Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara, wamefikishwa mbele ya Hakimu Mkazi, Bi. Agnes Futakamba, wa Mahakama ya Wilaya hiyo wakituhumiwa kwa kosa la ubadhilifu wa sh. milioni 12.32 zilizotolewa kwa ajili ya kuendesha mafunzo ya makuzi na malezi ya mtoto.

Washtakiwa hao ni Bw. Hassan Mwakipa ambaye ni Ofisa Tabibu Msaidizi na Mhasibu Bw. Absolum Ntakandi ambaye hakuwepo mahakamani ambao wankabiliwa na mashtaka 15.

Mwendesha Mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Bw. Sospeter Tyeah, alisema washtakiwa wote wanadaiwa kutenda makosa hayo kati ya Juni 11-16, 2009.

Alisema makosa hayo yamegawanyika katika maeneo matatu, ambayo ni kula njama za kumdanganya mwajiri wao na kubadilisha matumizi ya fedha kwa manufaa yao binafsi, kugushi nyaraka na kuhujumu uchumi.

Bw. Tyeah alisema katika kosa la kwanza, washtakiwa wanadaiwa
kutengeneza nyaraka za malipo ya washiriki 25 wa mafunzo ya makuzi na malezi ya mtoto Juni 11, 2009 na kila mmoja kulipwa sh. 320,000.

Kosa la pili, katika kipindi hicho washtakiwa wanadaiwa kutumia karatasi zisizo na tarehe kuwalipa washiriki saba sh. 450,000 kila mmoja maelezo ambayo ni ya uongo.

Mashtaka mengine ni kumlipa Bi. Elizabeth Macha, sh. 560,000 kwa madai ya kuhudhuria mafunzo hayo kama mwezeshaji na kuandaa stakabadhi namba R07584 ya Januari, 4, 2010.

Stakabadhi hiyo ilieleza kuwa, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo alimlipa Mkurugenzi wa Chuo cha Ushirika, tawi la Mtwara, sh. 129,000 kama gharama za ukumbi.

Bw. Tyeah ambaye alitumia zaidi ya dakika 20 kusoma tuhuma hizo, alidai washtakiwa walitumia tiketi ya ndege PW/MQQB7 ya Juni 9, 2009 wakidai ilitumiwa na Bi. Elizaberth Macha kwa ajili ya safari ambayo gharama yake ni sh. 368,000.

Stakabadhi nyingine haikuwa na tarehe ikionesha Mkurugenzi wa halmashauri hiyo alimlipa sh. 750,000, Mkuu wa Chuo cha Ushirika kwa ajili ya ukumbi.

Shtaka lingine ni kuwepo risiti inayoonesha Juni, 12, 2009,
Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo amemlipa mtu ambaye hakutajwa jina sh. 320,000 ili kununua karatasi kwa ajili ya kuendesha mafunzo hayo.

Bw. Tyeah aliieleza mahakama kuwa washtakiwa wanakabiliwa na mashtaka ya kugushi nyaraka, kubadilisha matumizi ya fedha na kuisababishia halmashauri hasara ya sh. milioni 12.32.

Mwisho.



No comments:

Post a Comment