Tuesday, September 05, 2017

MBUNGE AKEMEA WANAFUNZI KUMWAGIA UPUPU WAALIMU

Na Rose Itono,Mkuranga

MBUNGE wa Jimbo la Mkuranga Mkoa wa Pwani amelaani vikali tabia ya utovu wa nidhamu iliyooneshwa na wanafunzi wa shule ya Msingi Malela kwa kuwamwagia upupu ofisi za walimu wao na kuagiza tume iundwe ili kubaini chanzo cha tatizo hilo.

Akizungumza katika ziara yake ya kukagua shughuli mbalimbali za maendeleo na kuzungumza na wananchi wa kijiji hicho hivi karibuni Ulega alioneshwa kusikitishwa na hali aliyoikuta ya walimu kujikuna kutokana na upupu unaodaiwa kumwagwa ofisini hapo na wanafunzi wa shule hiyo.

Alisema lengo lililomfanya kupita katika shule hiyo lilikuwa ni kujua namna gani walimu hao wamekuwa wakifanya kazi zao na changamoto zinazowakabili,lakini cha ajabu ameshangazwa kukuta walimu hao wakiwa katika tafrani ya kujikuna kutokana na upupu uliomwagwa ofisini kwao na watu wanaodhaniwa kuwa ni wanafunzi.

"Mwenyekiti hakikisha unaunda timu ya haraka ambayo utashirikiana na diwani ili kubaini wahusika wa tukio hilo ambalo ni utovu wa nidhamu na kwamba atakayebainika kuhusika achukuliwe hatua za kinidhamu ili iwe fundisho kwa wengine,"alisema
Ulega aliongeza kuwataka wazazi na walezi wa watoto hao kushirikina na walimu katika kudumisha nidhamu kwani vitendo vya utovu wa nidhamu vinachangia kwa kiasi kikubwa kurudisdha nyuma maendeleo katika taifa.

Kwa upande wake mmoja wa walimu wa shule hiyo Theresia Mula alimweleza mbunge huyo kuwa shule yao imekuwa ikikabiliwa na changamoto mbalimbali za ukosefu wa vitendea kazi sambamba na mahusiano mabaya baina yao wazazi, walezi na wanafunzi.

Alisema wazazi na walezi wa wanafunzi wa kijiji hicho wamekuwa wakiwakataza watoto wao wasitumwe na walimu wao kitu ambacho kimewajenga wanafunzi kuwa na kiburi na kushindwa kuwaheshimu walimu wao wanapokuwa shuleni hata wanapokutana njiani.

"Ukimtuma maji au kitu chochote mwanafunzi anayesoma shuleni hapo mzazi anakuja juu hali ambayo inaonesha ni namna gani watoto hao wamekuwa wakipata misingi mibaya kutoka kwa wazazi na walezi wao,"alisema na kuongeza kuwa tabia hiyo ndiyo imekuwa ikiwafanya wanafunzi kupata kiburi na kumwaga upupu kwenye ofisi za walimu.

Pia Mwenyekiti wa kijiji hicho Mohamed Mbarami aliwasihi walimu wa shule hiyo kuacha tabia ya kukaa nje ya vituo vyao vya kazi badala yake waishi katika nyumba zilizojengwa kandokando ya shule ili kuleta ufanisi wa kazi.

"Ni vigumu mwalimu au mtumishi wa serikali anayekaa mbali na kituo chake cha kazi kuwa na ufanisi badala yake atabaki akichelewa kutokana na umbali uliopo baina ya shule na maeneo ya makazi,"alisisitiza

Mbunge huyo alifanya ziara katika kata tatu za wilaya hiyo ambazo ni kata ya vianzi, Vikindu na mwandege ili kuhamasisha shughuli za maendeleo na kusikiliza changamoto zinazowakabili wananchgi hao.

Mwisho.

No comments:

Post a Comment