Thursday, June 21, 2012

AFYA YAKARIBISHWA KUWEKEZA VIJIJINI



Na mwandishi wetu, aliyekuwa Shinyanga

Wananchi wa vijiji vya Mkoa wa Shinyanga wameiomba Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kuwasogezea huduma ya vituo vya afya ili wapate huduma hiyo kwa urahisi.

Wakizungumza na gazeti hili baadhi ya wakazi wa Kijiji cha Kishima Wilaya ya Kahama walisema kuwa, wamekuwa wakilazimika kutembea umbali mrefu kwa ajili ya kupata huduma.


Walisema kuwa, mbali na vituo hivyo kuwa mbali pia upatikanaji wa huduma bado hauridhishi na kufanya baadhi ya watu hasa wa kipato cha chini kushindwa kumudu gharama hizo.

Bi. Zena Khamis mkazi wa Kijiji hicho alisema tatizo hilo limekuwa likiwabana zaidi wanawake kutokana na mazimngira yao ya kipato.

Alisema, imefika wakati hata wale wagonjwa wanaokwenda vituo vya afya kwa ajili ya kupata huduma za dawa ya kurefusha maisha ARVs ni lazima watu watembee kwa muda mrefu kwa ajili ya kuchukua dawa.

"Kituo cha afya cha serikali kipo mbali hivyo kulingana na mazingira na elimu ndogo baadhi ya watu hujikuta wakikatisha kuchukua dawa hali ambayo inachangia kudhoofisha afya zao," alisema Bi. Khamis.

Mkazi wa Kijiji Cha Isagehe Bw. Festo Makambi alisema mbali na vituo kuwa mbali bado vijiji vyao vina uhaba wa upatikanaji wa madawa na kusanbabisha baadhi ya watu kutumia miti shamba.

Alisema, watu wamekuwa wakitumia miti shamba kutokana na kushindwa kumudu gharama za matibabu katika hospitali binafasi hivyo ni wajibu serikali ikaliangalia tatizo hilo na kulifanyia kazi.

Naye Mganga Mkuu wa Zahanati ya Kata ya Isagehe ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini, alipoulizwa hali halisi ya upatikanaji wa madawa na huduma kwa ujumla alikataa kuzungumzia masuala hayo kwa madai kuwa hana kibali cha kutoa ufafanuzi.

Alisema, wana barua rasmi inayowataka kutozungumza jambo lolote mpaka kwa Mganga Mkuu wa wilaya.

"Nendeni kwa Mganga Mkuu wa Wilaya ya Kahama atazungumza, lakini mimi siruhusiwi kabisa na nina barua rasmi inayoelekeza," alisema na kuongeza kuwa anashukuru hata manesi wake kutoongea kitu kwani ni kosa kisheria.



No comments:

Post a Comment