Tuesday, June 19, 2012

Taarifa ya Kuuaga Mwili wa Willy Edward

TAARIFA KUHUSU HESHIMA ZA MWISHO NA MAZISHI
YA ALIYEKUWA MHARIRI WA JAMBO LEO
MAREHEMU WILLY EDWARD OGUNDE

1.   Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) linapenda kuuarifu umma kwamba, shughuli za kuuaga (kutoa heshima za mwisho) kwa aliyekuwa Mhariri Mkuu wa gazeti la Jambo Leo na mwanachama wa TEF, Willy Edward Ogunde zitafanyika kesho, Jumatano Juni 20, 2012, katika viwanja vya Mnazimmoja (Arnatouglou) jijini Dar es Salaam.

2.   Shughuli hii ya mwanzo wa kuhitimisha safari ya mwisho ya mwenzetu, itafanyika kuanzia saa 4.00 asubuhi ikiongozwa na wanafamilia kwa kushirikiana na Kampuni ya Jambo Concept alikokuwa akifanya kazi Willy na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF).

3.   Baada ya shughuli za kutoa heshima za mwisho kukamilika, safari ya kuusafirisha mwili wa marehemu Willy kwenda Mugumu, Serengeti itaanza majira ya mchana kwa ajili ya mazishi yanayotarajiwa kufanyika Jumamosi, Juni 23, 2012 hukohuko Serengeti.

4.   Jukwaa la Wahariri katika mazishi hayo litawakilishwa na ujumbe wa watu wanne wakiongozwa na Mwenyekiti wa TEF, Absalom Kibanda, Mhariri Msanifu wa New Habari Ltd, Revocatus Makaranga na Mhariri Msanifu wa Magazeti ya Uhuru na Mzalengo, Jane Mihanji. Kadhalika Mkuu wa Wilaya ya Magu mkoani Mwanza, Jacqueline Liana ambaye alikuwa mwanachama wa TEF pia anatarajiwa kuungana na ujumbe huyo kwenye mazishi.

5.   TEF tukiwa tumeguswa sana na msiba huu, tunachukua fursa hii kuwashukuru wadau wetu wote ambao kwa namna moja au nyingine walitufariji, kutuma salaam za rambirambi nakutoa michango yao ya hali na mali tangu mauti yalipomkuta mwenzetu mkoani Morogoro usiku wa kuamkia Jumapili Juni 16, 2012 alikokuwa amekwenda kushiriki semina ya masuala ya Sensa ya Watu na Makazi ya 2012.

6.   Kwa uchache tunaomba shukrani zetu ziwafikie Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Joel Bendera, Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, waandishi wa habari wa mkoa wa Morogoro na Ofisi ya Taifa ya Sensa (NBS) ambao kwa namna moja au nyingine waliwezesha kusafirishwa kwa mwili wa marehemu kutoka Morgororo hadi hosipitali ya Taifa ya Muhimbili, Dar es Salaam.

7.   Pia tunawashukuru Kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL), Shirika la Nyumba la Taifa (NHC),

8.   Kwa mara nyingine tunawapa pole wale wote walioguswa kwa namna moja au nyingine na msiba huu wa ghafla, wakiwamo familia ya marehemu, hususan mke wake na watoto, wafanyakazi wa gazeti la Jambo Leo na wanahabari wote katika tasnia nzima ya habari nchini.

9.   Sisi katika Jukwaa la Wahariri tumeguswa kwa namna ya pekee na msiba huu mkubwa. Willy Edward Ogunde ametuacha na ametuachia majonzi makubwa, pia pengo kubwa katika fani ya habari. Kama tulivyosema katika taarifa yetuya awali, tunamshukuru Mungu aliyetupa nafasi ya kushirikiana naye katika maisha ya kitaaluma na zaidi tukiwa wahariri.

10. Kwa wale wanaosafiri kwenda Serengeti, tunawatakia Baraka za Mungu katika safari hiyo na Mungu awatangulie ili wakatuwakilishe vyema katika mazishi ya mwenzetu Willy Edward Ogunde. Bwana alitoa na Bwana ametwa jina lake lihimidiwe.

KATIBU WA JUKWAA LA WAHARIRI (TEF)




No comments:

Post a Comment