Wednesday, June 13, 2012

MAHANGA:WANAOTUMIKISHA WATOTO TUMEANZA KUWABANA


Na mwandishi wetu
SERIKALI imeanza kuchukulia hatua kwa taasisi, mashirika na watu mbalimbali wanaotumikisha watoto walio chini ya miaka 18 na kuwakosesha haki zao za msingi ikiwemo ya kupata elimu.

Naibu Waziri wa Kazi na Ajira, Dkt. Makongoro Mahanga, aliyasema hayo Dar es Salaam jana katika kilele cha Siku ya Kimataifa ya kupiga vita utumikishwaji watoto iliyoandaliwa na Shirika la Kazi Duniani (ILO).

Alisema tayari hatua za kisheria zimechukuliwa kwa watu wanaotumikisha watoto walio chini ya miaka 18, ambao  walichukuliwa na kupewa haki zao za msingi ikiwamo elimu.

Aliongeza kuwa, suala la malezi, matunzo na kuwalinda watoto dhidi ya vitendo vyote vinavyolenga kuhujumu haki zao ni jukumu la wadau wote kutokomeza vitendo hivyo.

“Utumikishwaji watoto katika kazi hatarishi ni hujuma kwa haki za mtoto kuishi, kukosa muda wa kupumzika, malezi bora, kucheza  na kupata elimu,” alisema Bw. Mahanga

Alisema utumikishwaji watoto ni tatizo la kitaifa na kimataifa, ambapo kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na ILO mwaka 2010, zinaonesha watoto milioni 215 wanatumikishwa katika sekta mbalimbali duniani kote.

“Katika Afrika nchi zilizo katika Jangwa la Sahara, zinakadiriwa kuwa na watoto milioni 65 wanaotumikishwa katika kazi za hatari, upande wa Tanzania kwa mujibu wa tafiti zilizofanywa mwaka 2005/2006, asilimia 18.7 ya watoto wenye umri kati ya miaka mitano hadi 17, wanatumikishwa katika shughuli mbalimbali,” alisema Dkt. Mahanga.

Aliongeza kuwa, Serikali kwa kushirikiana na wadau imeandaa na imeanza kutekeleza mpango kazi wa kitaifa wenye lengo la kutokomeza utumikishwaji watoto.

Mpango huo umelenga kutimiza malengo ya milenia ifikapo mwaka 2015 ambapo Serikali imefanikiwa kuandaa orodha ya kazi hatarishi ambazo hazipaswi kufanywa na watoto chini ya umri wa miaka 18.



No comments:

Post a Comment