Wednesday, June 13, 2012

MAJANGILI WANNE WANASWA WAKITEGA TEMBO KWA SUMU



Na mwandishi wetu

MAMLAKA ya Hifadhi ya Ngorongoro, mkoani Arusha,  imewakamata watu wanne wanaodhaniwa kuwa majangili ambao huwinda wanyama kwa kuwapa sumu katika msitu wa mamalaka hiyo ulioko eneo la Kambi ya Simba, wilayani Karatu.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Meneja Huduma za Uhifadhi wa mamlaka hiyo, Bw. Amiyo Amiyo, alisema watu hao walikamatwa juzi, saa ya nne asubuhi katika Msitu wa Sahata.

Alisema watu hao walikuwa na maboga 10 ambayo ndani yake waliyaweka sumu ya kuulia wanyama mbalimbali hasa tembo.

Aliongeza kuwa, hivi sasa majangili wamebadili mbinu ya kuwinda wanyama wakitumia sumu aina ya “aldicarb” ambayo kwa jina jingine hujulikana kama “temk”, kwa mujibu wa uchunguzi wa Mkemia Mkuu wa Serikali.

Bw. Amiyo alisema sumu hiyo ipo kwenye kundi la “Carbametes”, ambayo huathiri mfumo wa ufahamu wa mnyama kama wataila hivyo kusababisha kifo chake.

Katika tukio hilo, majangili hao walikutwa wakilinda maboga waliyotega msituni ili yasiliwe na wanyama wengine zaidi ya tembo ambapo kutokana na hali hiyo, mamlaka imelazimika kuimarisha ulinzi katika misitu.

“Kutokana na doria tunayoifanya kila siku, tumefanikiwa kukamata majangili hawa na kukuta mizoga ya tembo wawili ambao tayari walikuwa wametolewa meno,” alisema.

Alisema majangili hao wanafahamika kwa majina ya Bw. John Lohay (62),  Bw. John Amisi (27), Bw. Isaya Arusha (36), Bw. Roman Amsi (23) wote wakazi wa Kambiya Samba, wilayani Karatu na wamekabidhiwa kwa Jeshi la Polisi.

Aliongeza kuwa, Februali mwaka huu mamlaka hiyo ilifanikiwa kukamata watu wawili katika Msitu wa Mangola Juu wilayani Karatu wakiwa na matikiti maji 60 ndani ya msitu huo.

Alisema matikiti hayo yalikuwa na sumu ya iina hiyo na tayari wamefikishwa katika Mahakama ya Wilaya mjini Karatu.

“Kimsingi majangili wamebuni mbinu mpya ya kuwatega wanyama na kuwaua kwa kutumia sumu, tutahakikisha ulinzi unaimarishwa dani ya misitu yetu ili kupambana na hawa magangili,” alisema




No comments:

Post a Comment