Saturday, May 19, 2018

CRDB BANK YAJIPANGA KUKABILIANA NA USHINDANI


PICHANI: Viongozi Meza Kuu kwenye Mkutano Mkuu wa 23 wa Wanahisa wa Benki ya CRDB uliofanyika leo Mei 19, 2018. Mkutano huo umefanyika Ukumbi wa Simba (AICC) jijini Arusha. (Picha na Yusuph Mussa, Immamatukio Blog).

Na Yusuph Mussa, Immamatukio Blog, Arusha

TAASISI za fedha hasa mabenki yanakabiliwa na ushindani mkubwa kutokana na ongezeko la huduma za kifedha kutolewa na makampuni ya simu.

Suala hilo limechangia kwa kiasi kikubwa kufungwa kwa benki tano, huku nyingine tano zikiwa chini ya uangalizi maalumu.

Ili kukabiliana na ushindani huo, Benki ya CRDB imejipanga kukabiliana na ushindani huo kwa mwaka 2018 ili kuona inapata ufanisi. Na hiyo pia ni kutokana na Serikali kutoa fursa kadhaa kwa mabenki nchini kujiendesha kwa faida.

Hayo yamesemwa leo Mei 19, 2018 na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB Dkt. Charles Kimei wakati anasoma taarifa yake kwenye Mkutano Mkuu wa 23 wa Wanahisa wa Benki hiyo uliofanyika Ukumbi wa Simba (AICC) jijini Arusha.

"Kutokana na ushindani mkali kutoka taasisi zisizo za kifedha, hasa huduma za simu za mkononi na changamoto nyingine, benki nyingi ndogo zilikuwa na hali ngumu, na benki takribani tano zilifungwa na Benki Kuu, na benki nyingine tano ziliwekwa chini ya uangalizi maalumu.

"Ili kukabiliana na changamoto za ukwasi na kuongeza kasi ya ukuaji wa mikopo kwa sekta binafsi, Benki Kuu ilipunguza kiwango cha amana ya benki hadi kufikia asilimia nane (8) na kupunguza kiwango cha riba kwa mikopo ya benki za biashara kutoka asilimia 12 hadi tisa" alisema Dkt. Kimei.

Dkt. Kimei alisema kwa maana hiyo benki za biashara zina uwezo wa kukopa fedha hizo serikalini na wao kuweza kuwakopesha wafanya biashara na watu binafsi, hivyo kurudisha mzunguko wa fedha na shughuli za kawaida kwa wananchi.

Hivyo, Benki ya CRDB imejiwekea malengo ya kimkakati kwa mwaka 2018. Mpango mkakati huo wa miaka mitano 2018-2022, una lengo la kuifanya benki ya CRDB na kampuni zake tanzu kuongoza katika kupata faida kwa kukuza ubora wa rasilimali kupitia huduma kwa wateja.

Wateja hao ni wale binafsi, wadogo na wa kati, ikitumia huduma za kidijitali zenye ubora wa hali ya juu, huku wakiahidi kufanya mageuzi makubwa mwaka huu, katika matawi yao kwa lengo la kuongeza ufanisi na tija.

"Lengo kuu mwaka 2018 litakuwa ni kuongeza kasi ya mageuzi ya kidijitali na kupunguza kiwango cha mikopo chefuchefu (isiyo rudishwa kwa wakati) hadi asilimia nane, kuboresha wastani wa kiwango cha gharama na mapato hadi asilimia 58, na kufanya mageuzi ya uendeshaji kwenye matawi ya benki ili kuongeza tija na ufanisi" alisema Dkt. Kimei.


Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB Dkt. Charles Kimei akisoma taarifa yake ya mwaka kwenye Mkutano Mkuu wa 23 wa Wanahisa wa Benki hiyo leo Mei 19, 2018. Mkutano huo umefanyika Ukumbi wa Simba (AICC) jijini Arusha. (Picha na Yusuph Mussa, Immamatukio Blog).


Mkutano Mkuu wa 23 wa Wanahisa wa Benki ya CRDB uliofanyika leo Mei 19, 2018. Mkutano huo umefanyika Ukumbi wa Simba (AICC) jijini Arusha. (Picha na Yusuph Mussa, Immamatukio Blog).

No comments:

Post a Comment