Saturday, May 19, 2018

YAFUATAYO YATAKUSAIDIA KUFANIKISHA MFUNGO WA RAMADHANI

Na Jumia Travel Tanzania

Mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani umekaribia ambapo Waislamu wote nchini na duniani wanatarajiwa kuanza kufunga. Mwezi huu muhimu kiimani huchukuliwa kama kipindi cha toba ambapo waumini hufunga kwa kujinyima kula, kufanya ibada pamoja na kufanya matendo mema na ya huruma katika kipindi chote cha mfungo. 

Ikiwa zimebaki siku chache kabla ya kuanza kwa Ramadhani, Jumia Travel imekukusanyia mambo yafuatayo ya kufanya ndani ya kipindi hiki ili kukurahisishia kufanikishia mfungo wako.


Kamilisha funga zako. Mafundisho yanawataka waumini wafunge kwa imani na kwa moyo wote ili kupata thawabu kutoka kwa Mungu, ikiwemo dhambi zao kusamehewa. Kuna faida kubwa za kufunga ambazo zinatarajiwa baada ya kuisha kwa mfungo. Kwa hiyo, endapo utafunga hakikisha unafunga kwa moyo wote na dhamira ya dhati moyoni ili uje ulipwe kwa matendo yako.

Fanya matendo yatakayompendeza Mungu. Lengo kuu la Ramadhani ni kurudisha imani kwa mwenyezi Mungu kwa kuachana na anasa za dunia. Mfungo, kiasilia, utakusaidia kuyafanikisha hayo lakini utafanikiwa zaidi kwa kuyachunga matendo yako hususani yale yasiyompendeza muumba wako. Ni vema katika kipindi hiki kuwa unajikumbusha mara kwa mara kipindi chote cha mfungo, kwa kufanya hivyo utaogopa kutenda au kufikiria maovu.

Soma Quran. Ramadhani ni mwezi wa Quran. Itakuwa haujaitendea haki na ni kazi bure kama hautokisoma kitabu hiki kitukufu. Hii hapa ni njia rahisi unayoweza kuifuata. Kwa kuwa utakuwa unafunga, maana yake utakuwa huru muda wa chakula cha mchana. Utumie muda huo kusoma. Kama hauna kitabu, mambo yamerahisishwa kupitia teknolojia siku hizi. Unaweza kupakua programu ya simu ya mkononi na kujisomea. Hii ni njia rahisi na inayowezekana ya kujisomea Quran.

Chunga ulimi wako. Njia mojawapo rahisi inayoweza kuharibu funga yako ni kwa kujihusisha na umbeya na maongezi yasiyompendeza Mungu. Mwenyezi Mungu hamuhitaji mtu ambaye hataki kuachana na mienendo yake miovu katika kipindi cha mfungo. Hivyo basi, kwa mwaka huu, jitahidi kwa kadri uwezavyo kukaa mbali au kujiepusha na maongezi ambayo yatakupelekea kumkosea muumba wako.

Toa msaada. Mtume Muhammad (SAW), alikuwa akijulikana kama mtu mwenye ukarimu wa hali ya juu, lakini kipindi cha mwezi wa Ramadhani ukarimu wake uliongezeka kupita kiwango. Ramadhani inakupatia fursa pekee ya kuongeza moyo wako wa kujitolea ili kujiongezea thawabu zaidi. Kwa kuongezea, utakuwa unafanya kama vile alivyofanya mtume wa Mungu. Kwa hiyo, hakikisha unawasaidia watu mbalimbali wasiojiweza na kuhitaji msaada katika kipindi hiki cha mfungo.

Ramadhani ni kipindi muhimu cha kujitafakari kiimani, kujiimarisha na kujitoa kwa waumini wa dini ya Kiislamu. Jumia Travel ingependa kuwatakiwa Waislamu wote maandalizi ya mfungo mwema wa mwezi mtukufu wa Ramadhani na kuyazingatia mafundisho na yale yote yaliyoagizwa ili kumaliza salama.


No comments:

Post a Comment