Saturday, March 24, 2018

UPDATE: MAWASILIANO YA BARABARA YA ITIGI HADI TABORA YAREJEA

PICHANI : Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Elias Kwandikwa(kulia) na Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS) Mkoa wa Tabora, Mhandisi Damian Ndabalinze (kushoto) wakikagua ukarabati wa eneo Nyahua ambalo lilikuwa limekatika kwa sababu ya maji ya mvua na kusababisha kukatika kwa mawasiliano baina ya Itiga na Tabora jana wilayani Uyui.


NA TIGANYA VINCENT
RS TABORA

HATIMAYE Mawasiliano ya barabara ya Tabora kupitia Itigi hadi Dodoma yalikuwa yamekatika kutokana na maji ya mvua kubwa iliyonyesha na kusababisha kipande cha barabara kukatika katika eneo la Nyahua wilayani Uyui yamerejea.

Akizungumza jana katika eneo Nyahua ambalo barabara ilikuwa imekatika Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Elias Kwandikwa aliipongeza Kampuni ya CHICO kwa kushiriana na Wakala wa Barabara Tanzania Mkoani Tabora kwa kurejesha haraka hali ya mawasiliano katika eneo hilo.

Alisema jitihada zilifanywa za kurudisha mawasiliano ili magari yaanze tena kutumia barabara hiyo zinatia moyo na kuzitaka Kampuni nyingine za ujenzi hapa nchini kunapotea tatizo la aina yoyote katika barabara kuwa tayari kushirikiana na Serikali katika kuhakikisha wananchi wanaendelea kusafiri bila usumbufu.

Kwandikwa alisema barabara hiyo kuanza kutumika tena kumepunguza gharama za matumizi ya mafuta kwa wenye magari kwa kuwa walipokuwa wakizungukia Nzega ziliongezeka Kilometa karibu 200 na hivyo kuongeza pia muda wa kusafiri.

Hata hivyo Naibu Waziri huyo alitoa tahadhari kwa madereva wa magari ya abiria na mizigo kuwa makini wanapopita eneo lilikuwa limekatika kwa sababu yapo maeneo ambayo yanaoonyesha maji yalichimba chini kwa chini wakati yakitafuta upenyo ili kuepuka kusababisha maafa au hasara za kupoteza mizigo.

Kwandikwa alitoa wito kwa wasafiri na madereva kuwa wanakubaliana na mazuio pindi kunapotekea na matatizo katika barabara kwa kuwa Serikali nia yake ni kuhakikisha hakuna madhara yanayoweza kusababisha na matatizo yoyote katika barabara.

Aidha Naibu Waziri huyo alisema kuwa tayari Mkandarasi yuko katika eneo la Mradi ili kukamilisha kipande hicho chenye urefu wa Kilometa 85 ambacho kitajengwa kwa kiwango cha lami kwa gharama ya bilioni 117 ikiwa ni pamoja na ujenzi wa madaraja katika eneo hilo korofi.

Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS) Mkoa wa Tabora, Mhandisi Damian Ndabalinze alisema Mkandarasi amejitahidi kufanya kazi hiyo ya dhararua kwa haraka zaidi na kuwezesha magari kuanza tena kupita katika eneo hilo.

Aliwataka madreva wa magari wanapoambiwa kupitia sehemu fulani wakati wa dhararu wasidharau ili wasije wakasababisha hasara katika mali zao na kupoteza maisha ya watu.

Naye Mmjoa wa Wasafiri kijiji cha Mwamabondo Kata ya Loya Jondia Masalu alisema alishindwa kuendelea na safari yake kwa sababu ya kukatika kwa barabara hiyo katika eneo hilo la Nyahua na kusababisha kuendelea kuwepo Tabora mjini na hivyo kuongeza gharama za kupanga na chakula.

Alisema juhudi zilizofanywa na Serikali kupitia TANROADS zimsaidia kuanza safari ya kurejea kwake na uhakika wa kufika salama.

Eneo hilo la Nyahua lilikatika juzi na kusababisha magari ya mizigo na abiria kuanza kupitia Nzega ambapo ni mbali kufika Tabora kwa kutumia njia hiyo./

Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Elias Kwandikwa alichungulia moja ya mashimo katika eneo la Nyahua lilosababishwa na maji ya mvua yaliyokata kipande hicho cha barabara ya Itigi hadi Tabora jana wakati alipotembelea kujionea madhara yaliyojitokeza na mipango ya ukarabati.


Mkuu wa Matengenezo wa Wakala wa Barabara Tanzania9 TANROADS) Mkoani Raphael Mlimaji (Kulia) akimwonyesha jana Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Elias Kwandikwa (kushoto) shimo lililosababishwa na mvua iliyokata sehemu ya barabara katika eneo la Nyahua na kusababisha mawasiliano Itigi hadi Tabora jana na kukatika.


Baadhi ya watumiaji wa barabara ya Itigi hadi Tabora wakikatisha eneo mablo lilikuwa halipitiki baada ya ukarabati wa eneo hilo uliofanywa na TANROADS kwa ushirikiano na Kampuni ya CHICO.


Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Elias Kwandikwa(kulia) akiongea na waandishi wa habari jana katika eneo la Nyahua wilayani Uyui baada ya kutembelea eneo hilo ambalo lilikuwa limekatika kutokana na mvua kubwa iliyonyesha na kukata sehemu ya barabara. Kushoto ni Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS) Mkoa wa Tabora, Mhandisi Damian Ndabalinze .

Picha zote na Tiganya Vincent

No comments:

Post a Comment