Monday, October 05, 2015

MAJAMBAZI SITA YAKAMATWA KWA MAUAJI YA AFISA WA POLISI DAR

JESHI la Polisi Kanda maalum ya Dar es Salaam limewakamata majambazi sugu sita waliohusika kumuua Afisa wa Polisi ASP Elibariki Pallangyo, aliyekuwa akifanya kazi katika kikosi maalum cha kupambana na majambazi.

Hayo yamesemwa leo jijini Dar es Salaam na Kamishna wa Polisi kanda maalum ya Dar es Salaam,Suleiman Kova ambapo alisema kuwa majambazi hao wanaongozwa na Omary Salehe maarufu kama Bonge Mzito walifanya tukio hilo Agosti 4 mwaka huu nyumbani kwa Marehemu huko Yombo.

Kova amewataja majambazi hao kuwa ni Omary Salehe (39), Saidi Saidi Mzee (37),Rashid Waston(21),Ramadhan Salum (38),Bakari Salim Rashid (38), na Hamisi Hamisi (24) ambao wote walikubali kuhusika katika mauwaji hayo kwa makusudi.

Amesema kuwa majambazi hao walienda kwa ASP Pallangyo na kumvamia usiku wa manane akiwa amelala na familia yake na kumuua mbele ya familia nzima ikishuhudia.

Anaongeza kuwa mtuhumiwa namba moja Bw Salehe alikutwa na bastola aina ya Revolver iliyofutwa namba na baada ya kuhojiwa alidai kuwa silaha hiyo ndiyo iliyotumika katika tukio hilo.

Kamishna Kova amesema mtuhumiwa huyo alijaribu kuwa toroka Polisi kwa kuwadanganya kuwa ameficha silaha nyingine mahali na kutaka kukimbia lakini polisi walimuwahi na kumpiga risasi iliyopelekea akutwe na umauti.

"Mtuhumiwa mwingine huyu  Waston tumemkamata na silaha aina ya Shortgun iliyokatwa mtutu ambayo waliitengeneza kihenyeji ikiwa na risasi nne na betri nne zilizounganishwa kwaajili ya kulipua baruti,"amesema Kova

Katika tukio lingine Jeshi la Polisi limefanikiwa kuwakamata watuhumiwa wengine saba wa ujambazi wanaojihusisha na kuratibu matukio ya uvamizi wa vituo vya polisi pamoja na ugaidi ambao watano kati yao ni familia moja ya ukoo wa Ulatule.

Kamanda Kova amesema kuwa watuhumiwa hao wanahusika na matukio ya kupanga na kuratibu uvamizi wa vituo vya polisi ambapo pia wamekuwa wakiendesha kambi za mafunzo huko mkoani Morogoro kwa kutumia fedha walizokuwa wakijipatia kwa njia ya udanganyifu.

Amewataja watuhumiwa hao kuwa ni Siad Mohamed Ulatule (67),Ramadhan Ally Ngande(29),Hamis Mohamed Salum Simba Ulatule (51),Ally Mohamed Salum Simba Ulatule (65),Nassor Suleiman Ulatule (40),Seleman Abdallah Salum Ulatule (83) na Said Abdullah Chambeta (40).

"Jeshi la polisi limefanya operesheni hii kuhakikisha tunakomesha kabisa vitendo vya uvamizi wa vituo vya polisi pia tuna lengo la kuwaondolea wananchi hofu ya vitendo vya kigaidi nchini,"amesema Kova.No comments:

Post a Comment