Tuesday, June 03, 2014

UTAFITI WA GESI TANZANIA: WENGI WANAAMINI MATAJIRI NA SERIKALI NDIO WATANUFAIKA

Wananchi wanne kati ya watano wanaamini kuwa mafuta na gesi yatawanufaisha wao, watoto wao na nchi yao kwa ujumla. Wakati huo huo, wananchi wanne kati ya kumi (37%) wanaamini kuwa viongozi wa Serikali na matajiri ndio wataofaidika zaidi. Pia, zaidi ya nusu (55%) wangependa baadhi ya mapato ya mafuta na gesi wapewe wananchi moja kwa moja kama fedha taslimu.

Matokeo haya yametolewa na Twaweza katika muhtasari wa utafiti wenye jina la Kusimamia Maliasili: Wananchi wanasemaje?Utafiti huu ulifanywa kwa kushirikiana na Benki ya Dunia na umetokana na takwimu za Sauti za Wananchi, utafiti wa kwanza Afrika kwa njia ya simu ya mkononi wenye uwakilishi wa kitaifa.

Utafiti unaonesha kwamba matakwa ya wananchi ni kuwa, angalau kiasi cha mapato ya mafuta na gesi kipelekwe moja kwa moja kwa wananchi. Mwananchi mmoja kati ya watano (20%) angependelea kiasi kikubwa cha fedha kipelekwa moja kwa moja kwa wananchi; wakati wananchi asilimia 18 wangependelea kuwe na mgawo sawa wa mapato kati ya serikali na wananchi. Asilimia 17 wangependelea Serikali ipate asilimia kubwa zaidi ya mapato kwa ajili ya kuendeleza miundombinu na huduma za kijamii na wananchi wapewe kiasi kinachobaki.

Hata hivyo, Watanzania walio wengi (43%) wangependa mapato yote yaende Serikalini kwa ajili ya kugharamia huduma muhimu. Isitoshe, wananchi walipoulizwa namna wanavyoamini mapato ya rasilimali yanaweza kuleta manufaa kwa Watanzania, nusu yao (46%) walisema mapato yatumike katika kutoa huduma za afya na elimu, na wananchi wanne kati ya kumi (20%) walipendekeza yatumike kwenye miundombinu au kwenye mipango ya kupambana na umaskini (17%).

Linapokuja suala la usimamizi wa maliasili, jambo la msingi ni kuhakikisha kuwa Tanzania haiangukii kwenye uhanga wa laana ya utajiri wa maliasili. Uzoefu kutoka nchi nyingine unaonyesha kuwepo kwa uwazi kuhusu mapato na mchakato kama kitu muhimu sana katika kuepuka laana hii, pamoja na ushiriki wa wananchi katika kufanya maamuzi yanayohusu namna mapato yanavyosimamiwa.

Hivi sasa, ingawa Watanzania wengi (64%) wanafahamu ugunduzi wa mafuta na gesi, Utafiti wa Sauti za Wananchi ulibaini kuwa Watanzania wawili kati ya watatu (65%) wangependa kupata taarifa zaidi. Pindi taarifa zinapokosekana, tetesi na uvumi mara nyingi huziba pengo hilo. Ingawa makadirio ya sasa yanasema kuwa uchimbaji mkubwa wa mafuta na gesi hautaleta faida katika kipindi cha miaka saba hadi kumi ijayo, mwananchi mmoja kati ya watatu (36%) anaamini kuwa makampuni ya mafuta na gesi tayari yameshaanza kupata fedha kutokana na ugunduzi huu. Isitoshe wananchi watatu kati ya kumi (28%) hawana uhakika kama tayari kuna mapato kutoka kwenye mafuta na gesi au la. Aina hii ya mapengo kati ya mitazamo na uhalisia, kama haitaangaliwa vizuri, inaweza kusababisha wananchi kutoridhishwa na usimamizi wa maliasili.

Mjadala mwingine mkali umekuwa juu ya nafasi ya makampuni ya ndani na ya nje ya nchi katika kuchimba mafuta na gesi. Wafabiashara wengi wamedai kwa msisitizo upendeleo utolewe kwa makampuni ya Tanzania. Nusu ya Watanzania (52%) wangependa kunufaika na utaalamu wa makampuni ya kigeni katika sekta hii, lakini kwa kushirikiana na makampuni ya ndani ambayo yanapaswa kumiliki hisa kubwa zaidi katika ushirikiano wa kibiashara hio. Mwananchi mmoja kati ya watatu (35%) anaamini kuwa makampuni ya ndani yapewe kipaumbele kwenye zabuni za makubaliano. Aidha, Watanzania sita kati ya kumi (61%) wako tayari kuona mafuta na gesi yakiuzwa kimataifa kwenye nchi zote. Hata hivyo, wananchi watatu kati ya kumi (28%) wanafikiri gesi inapaswa kutumika nchini tu, na mwananchi mmoja tu kati ya ishirini (5%) anafikiri mauzo ya gesi yafanyike nchi za Afrika Mashariki pekee.

Rakesh Rajani, Mkuu wa Twaweza, alisema "Kama tunataka watu wa Tanzania wanufaike na ugunduzi wa gesi, tunahitaji uongozi wa serikali ulio imara, wenye uwazi na ubunifu. Kuwepo kwa mfuko huru wa utajiri wa taifa ni sehemu moja muhimu ya ufumbuzi. Hata hivyo, tunahitaji kufikiria juu ya njia mbadala, kama vile kupeleka fedha moja kwa moja kwa watu. Jambo la msingi zaidi ni kuweka wazi taarifa, kusikiliza maoni ya wananchi na kuwasiliana ili kujenga imani ya wananchi kufahamu namna fedha za gesi inavyotumika."

No comments:

Post a Comment