Wednesday, April 02, 2014

JOHN MNYIKA ANENA KUHUSU BODABODA NA BAJAJI JIJINI



TAARIFA KWA UMMA



Tangu tarehe 3/3/2014 Serikali kupitia kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Ndugu Meck Sadiq ilipotoa tamko la kupiga marufuku biashara ya kusafirisha abiria maeneo ya mijini kwa kutumia usafiri wa bodaboda na bajaji kumekuwa na mgogoro baina ya vijana wanaofanya kazi hiyo kwa upande mmoja na vyombo vya ulinzi na usalama kwa upande mwingine.

SOMA ZAIDI. . .


Aidha, kufuatia kauli hiyo watumiaji wa kawaida wa pikipiki na bajaji nao wamekuwa wakipata usumbufu wa kukamatwa kamatwa na kusumbuliwa wakidhaniwa kwamba ni sehemu ya biashara ya usafiri kwa kutumia bodaboda na bajaji.

Kadhalika, kuanza tamko hilo limezusha usumbufu kwa abiria ambao walikuwa wakitumia vyombo hivyo vya usafiri kama mbadala wakati huu ambapo ujenzi wa miundombinu ya Mabasi yaendayo kwa Haraka (BRT) imeambatana na ongezeko la foleni katika barabara zinazoelekea mjini.

Kwa upande mwingine pamekuwepo na utata kuhusu mipaka ya Eneo la Katikati ya Mji (Central Business District- CBD) linaloguswa na amri hiyo.

Kwa kuwa takribani mwezi mmoja umepita bila mgogoro huo kupatiwa ufumbuzi na Serikali yenyewe, nimeamua kuingilia kati ikiwa ni sehemu ya wajibu wa kibunge wa kuwakilisha wananchi na kuisimamia Serikali.

Hata hivyo, kwa kuwa nipo katika Mkutano wa Bunge Maalum la Katiba unaoendelea Dodoma ambapo sasa tupo katika hatua muhimu ya kupitia sura ya kwanza na sita za rasimu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zinazohusu Muundo wa Muungano na Mamlaka ya Wananchi nitaanza kwa hatua zifuatazo:

Mosi, Ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Ubungo kupitia kwa Katibu Msaidizi Aziz Himbuka tayari imeshafanya mawasiliano na Viongozi wa Waendesha Bodaboda katika Manispaa ya Kinondoni kwa ajili ya kupata maelezo na vielelezo kwa ajili ya kuchukua hatua zaidi.

Pili, nimemuandikia ujumbe mkuu wa Mkuu wa Mkoa Mecky Said kusitisha kwa muda utekelezaji wa tamko alilotoa ili kupisha mazungumzo baina ya Serikali, wahusika wa Bodaboda na Bajaji na wadau wengine muhimu ili kupata ufumbuzi.

Tatu, nimemwelekeza Katibu Msaidizi wa Mbunge aende ofisi za Mamlaka ya Usafiri wa Nchi Kavu na Madini (SUMATRA) kwa ajili ya kupata nakala ya kanuni na maagizo ili kutafakari iwapo misingi ya ushirikishwaji, haki na uhuru wa kisheria na kikatiba imezingatiwa katika mchakato mzima.

Nne, natoa mwito kwa Halmashauri ya Jiji na Manispaa za Ilala na Kinondoni kuweka wazi mipaka ya eneo la katikati ya Jiji (CBD) na pia kuweka utaratibu bora zaidi wa usafiri wa kuingia katikati ya mji wenye kuzingatia maslahi ya wasafiri wa Jiji wa Dar Es Salaam na fursa ya vijana kuweza kujiajiri.

Tano, natambua matatizo ya kushamiri kwa ajali za barabarani zinazohusisha waendeshaji wa bodaboda na bajaji na uhalifu unaohusisha matumizi ya vyombo hivyo vya usafiri, hata hivyo kupiga marufuku vyombo hivyo vya usafiri kuingia katikati ya mji katika eneo pana mpaka makazi ya watu wengi kuanzia Magomeni mpaka Ubungo sio ufumbuzi wa matatizo hayo.

Wenu katika uwakilishi wa wananchi,





John Mnyika



02/04/2014


No comments:

Post a Comment