Moshi,
Kesi ya usafirishaji wanyama hai kwenda Uarabuni
imeshindwa kuendelea kwa mara nyingine katika mahakama ya hakimu mkazi mjini
Moshi huku upande wa Jamhuri ukiomba kutolewa kwa hati ya kukamatwa kwa
mshtakiwa wa kwanza Kamran Ahmed ambaye hakufika mahakamani.
Ombi la kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo limetolewa na
mawakili wa Jamhuri, Evatha Mushin na Joseph Maugo baada ya mshtakiwa huyo
pamoja na wakili wake Edmundi Ngemela kutofika mahakamani bila maelezo
yoyote.
Mbele ya hakimu mkazi wa mahakama hiyo Simon Kobelo
mawakili hao walidai mshtakiwa huyo hafiki mahakamani hapo kwa makusudi na
kutaka awasilishe vyeti vya kupata matibabu hospitalini ambapo Feb. 26 mwaka
huu kupitia kwa wakili wake Ngemela aliomba kuahirishwa kwa kesi hiyo kutokana
na kupanda kwa sukari yake.
Mawakili hao waliiomba mahakama kukamatwa kwa mshtakiwa
huyo ambaye amekuwa akiisababishia hasara upande wa jamhuri kutokana na kuleta
mashahidi na kuwarejesha bila ya kutoa ushahidi wao mahakamani hapo.
Kesi hiyo ambayo ilifika mahakamani hapo kwa ajili ya
shahidi wa 22 kutoa ushahidi wake ililazimika kusubiriwa kwa zaidi ya masaa
sita hadi ilipoahirishwa katika mahakama ya ndani(Chamber Court) itaendelea
tena leo(MACHI 25) mwaka huu.
Hata hivyo pamoja na washitakiwa wengine watatu katika
kesi hiyo Hawa mang'unyuka, Martin Kimath na Michael Mrutu wanashitakiwa kwa
tuhuma za kusafirisha ndege na wanyama hao wakiwemo twiga wane wanaogharimu
dola za kimarekani zaidi ya 113, 715 mnamo Novemba 26 2010.
Katika kesi hiyo inayofuatiliwa na mamilioni ya
watanzania, shahidi wa 20, Robert Nyanda alieleza mahakama alivyomtambua
mshtakiwa wa kwanza(Ahmed) siku ya
tukio.
Shahidi huyo alidai siku ya tukio alishiriki katika
uandaaji wa vifaa kwa ajili ya upakiaji wa mizigo mizito katika ndege ikiwa ni
maelekezo ya bosi wake Rosemery Israel ambapo pia alishuhudia gari aina ya Fuso
likiwa limepakia maboksi yenye wanyama hao.
Kwa upande wake,shahidi wa 21 katika kesi hiyo,Rewald
Amani aliyekuwa meneja muongozaji wa ndege katika uwanja wa Kia,aliieleza
mahakama kuwa ndege hiyo ilitua nchini Novemba 24, 2010 katika kiwanja hicho na kuondoka Novemba 26,
2010 ikiwa salama kuelekea Doha Qatar.
No comments:
Post a Comment