Thursday, February 13, 2014

BREAKING NEWS: SUALA LA OKWI NA YANGA LIMEKWISHA, SOMA HAPA

Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) limemuidhinisha mshambuliaji Mganda, Emmanuel Okwi kuchezea klabu ya Yanga ya Dar es Salaam .

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi Dar es Salaam leo, Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Celestine Mwesiga alisema kesi iliyokuwa FIFA ni kuhusu ufafanuzi wa OKwi aliyekuwa SC Villa ya Uganda kwa mkopo kama anaweza kuichezea Yanga.

"FIFA wametoa ufafanuzi wa suala hilo ambapo wamesema kuwa kesi ya Okwi kutoka SC Villa ya Uganda kwenda Yanga hayo ni maisha binafsi ya mchezaji hivyo ilikuwa ni maamuzi yake mwenyewe kwa sababu FUFA (Chama cha Soka Uganda), kilitoa baraka zake," alisema Mwesiga.

SOMA ZAIDI...

Alisema hukusu Simba madai yao kwa Etoile du Sahel ya Tunisia yapo palepale kwani wana haki ya kudai lakini si kumzuia Okwi kwenda Yanga au klabu yeyote ambayo ingemhitaji.

Awali Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF iliyokutana Januari 22, mwaka huu kupitia masuala mbalimbali, ilisimamisha usajili wa Okwi baada ya kubaini kuwa mchezaji huyo aliruhusiwa kuichezea SC Villa ya Uganda kwa kibali maalumu kutoka FIFA.

Okwi ambaye aliingia mgogoro na klabu yake ya Etoile du Sahel ya Tunisia aliruhusiwa na FIFA kuchezea SC Villa kwa kibali maalumu (provisional permit) cha miezi sita ili kulinda kiwango chake wakati suala lake dhidi ya Etoile du Sahel likishughulikiwa na shirikisho hilo la kimataifa.

FIFA kulikuwa na kesi tatu kuhusiana na suala la mchezaji huyo. Wakati Okwi aliishitaki klabu hiyo FIFA kwa kutomlipa mshahara, Etoile du Sahel imemshitaki mchezaji huyo kwa utoro. Nayo Simba iliishitaki Etoile du Sahel kwa kushindwa kuilipa ada ya mauzo ya mchezaji huyo ambayo ni dola za Marekani 300,000.

Hivyo, TFF iliandikia FIFA kutaka kujua iwapo mchezaji huyo anaweza kucheza Ligi Kuu Tanzania wakati Etoile du Sahel ikiwa imefungua kesi katika shirikisho hilo la kimataifa ikidai Okwi bado ni mchezaji wake.

Kwa hali hiyo Okwi anaweza kuendelea kuicheza klabu yake mpya ya Yanga katika ligi kuu bara na michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.



No comments:

Post a Comment