Friday, January 10, 2014

NEWS: ABIRIA 1600 WAANDAMANA KUSHINIKIZA USAFIRI

Dodoma.

Zaidi ya abiria 1600 waliokuwa wakisafiri kwa kutumia reli ya kati kutoka mkoani Kigoma kwenda mikoa ya Morogoro na Dar es Salaam juzi waliandamana kuelekea katika ofisi za Mkuu wa Mkoa wa Dodoma wakipinga safari yao kusitishwa na Shirika la reli Tanzania(TRL) kutokana na kuharibika kwa reli eneo la Gulwe na Godegode wilayani Mpwapwa.

Akizungumza kwa niaba ya wenzake mbele ya mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt, Rehema Nchimbi mmoja wa abiria hao aliyejitambulisha kwa jina la Alphonce Evarist alisema kuwa wameshakaa njiani kwa muda wa siku nane tangu watoke Kigoma kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ya reli ya Dodoma kuharibika kwa kusombwa na maji yaliyotokana na mvua zinazoendelea kunyesha.

“Tukiwa Kigoma tuliahirishiwa safari kwa madai kuwa reli ya hapa Dodoma imeharibika kwa kusombwa na maji ya mvua sasa na tulipofika hapa tukaambiwa kuwa bado wanatengeneza reli sasa ni reli gani hiyo ambayo inatengenezwa kwa muda wa siku saba?”alihoji Evaristi.

Aliongeza kuwa abiria wengi wamepoteza mali zao ikiwemo mizigo na pesa hata kukosa chakula pamoja na kuuza baadhi ya vitu vyao ili kununua jambo ambalo limekuwa kikwazo kwao kutokana na kuishiwa na pesa pamoja na vitu vya kuuza ili kuweza kujikimu kwa chakula.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt, Rehema Nchimbi alikiri kuwepo kwa tatizo la kuharibika kwa reli hiyo katika eneo la Gulwe na Godegode lililoko katika Wilaya ya Mpwapwa na kusema kuwa hici karibuni reli hiyo ilitengenezwa na treni kuendelea na safari lakini kumetokea na uharibifu huo kwa mara nyingine ambapo wahusika wanalishughulikia tatizo hilo.

“Kipande cha reli katika eneo la Gulwe na Godegode ni moja kati ya eneo korofi sana kwakuwa mara nyingi huwa hukumbwa na mafuriko na ni kweli walishatengeneza hivi karibuni na baada ya matengenezo yalitokea mafuriko mengine na kusomba reli hiyo kwa mara nyingine tena,” alisema Dkt, Nchimbi.

Hata hivyo aliiagiza kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya ya Dodoma mjini kwa kushirikiana na uongozi wa TRL kuhakikisha zinaangalia usalama wa abiria hao kwa kipindi chote watakapokuwa mkoani hapa hadi usafiri wao utakapopatikana mara baada ya TRL kukamilisha matengenezo yao.

Aidha aliuagiza uongozi wa TRL kuhakikisha abiria wote wanapata huduma zote mihumu bure ikiwemo ya chakula na maliwato hadi hapo watakapo anza safari yao kwakuwa kwa wakati huo hapakuwa na usafiri wa magari ya kuwafikisha wanapokwenda kutokana na magari yote kuondoka hivyo hapakuwa na magari ya kutosha kuwarejesha makwao na kuwataka wavumilie hadi huo muda waliopewa na TRL.



Kwa upande wake Mhandisi Mitambo kutoka TRL mkoa wa Dodoma John Mandalu aliahidi kuwasaidia abiria hao huduma za chakula hadi safari yao itakapokuwa tayari kuanza na kuahidi hadi kufika saa 11 jioni ya jana tayari safari yao itaanza.

No comments:

Post a Comment