Friday, January 10, 2014

ACHA TU:JAMANI SHINYANGA NI BALAA…ONA HII

Shinyanga

Mkazi wa kijiji cha Ibelansuha kata ya ushetu wilayani Kahama mkoa wa Shinyanga amekufa papo hapo baada ya mdeni wake aliyekuwa akimdai kiasi cha shilingi 3,000 kumpiga na mpini wa jembe sehemu za ubavuni.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Shinyanga, Evarist Mangala amemtaja aliyekufa kuwa ni Magulu Mhangwa (35) na kwamba tukio hilo limetokea Januari 5, mwaka huu saa 2.00 asubuhi huko kijijini Ibelansuha wilayani Kahama.

Akifafanua kamanda Mangala alisema siku hiyo ya tukio Mhangwa alimfuata mtu mmoja aliyetambuliwa kwa jina moja la Majaliwa kwa ajili ya kudai fedha alizokuwa amemkopesha kiasi cha shilingi 3,000 ambapo baada kudaiwa fedha hizo alichukua uamuzi wa kumshambulia mdai wake.

SOMA ZAIDI...

“Mhangwa siku hiyo alimfuata huyo mtu aliyekuwa amemkopesha fedha zake na kumuomba amlipe deni hilo, lakini jambo la kusikitisha, mdaiwa alishikwa na hasira za kudaiwa ndipo alipookota mpini wa jembe na kumpiga nao mdai wake sehemu za ubavuni na kusababisha kifo chake papo hapo,” alieleza Mangala.

Kamanda Mangala alisema mara baada ya mtuhumiwa huyo kubaini Mhangwa amekufa alitoroka na kwenda kusikojulikana ambapo hivi sasa polisi inaendelea na msako wa kumtafuta ili aweze kukamatwa na kufikishwa mahakamani.

Katika tukio lingine mwanafunzi mwenye umri wa miaka minane aliyekuwa akisoma darasa la kwanza katika shule ya msingi Buchambi wilayani Kishapu mkoani Shinyanga, Paschal Mahembo amekufa papo hapo baada ya kugongwa na gari lililokuwa katika mwendo kasi.

Kamanda Mangala alisema ajali hiyo ilitokea juzi saa 5.45 asubuhi huko katika barabara ya Shinyanga kuelekea Mwanza eneo la kijiji cha Buchambi wilayani Kishapu wakati mwanafunzi huyo alipokuwa akikatisha barabara.

Alilitaja gari lililosababisha kifo hicho kuwa ni lenye namba za usajili T. 398 BKA Toyota Land cruiser mali ya kampuni ya Salum Transport Ltd. ya wilayani Nzega mkoa wa Tabora likiendeshwa na dereva aliyetajwa kwa jina la Paulo Michael (30).

Kamanda Mangala alisema uchunguzi wa awali umebaini kuwa chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi wa dereva wa gari hilo alipokuwa akitokea wilayani Bariadi mkoa wa Simiyu akielekea Nzega na kwamba uchunguzi wa kina unaendelea.


No comments:

Post a Comment