Wednesday, January 22, 2014

MABOMU ST. JOSEPH UNIVERSITY SONGEA, 40 MBARONI


Songea.

Jeshi la Polisi mkoani Ruvuma limelazimika kutumia nguvu kwa lengo la kuwatawanya wanafunzi wa chuo kikuu cha St. Joseph tawi la Songea kwa kupigwa na mabomu ya machozi baada ya wanafunzi hao kuandamana na kutaka kuingia kwenye eneo la chuo ambacho kilishafungwa tangu Januari 15 mwaka huu na kusababisha wanafunzi 40 kutiwa mbaroni akiwemo raisi wa serikali ya wanafunzi .

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma Deusdedit Nsimeki aliwaambia waandishi wa habari jana mchana kuwa tukio hilo lilitokea Januari 21 mwaka huu majira ya saa 2 asubuhi huko kwenye eneo la ruhuwiko katika manispaa ya Songea.

Alisema kuwa inadaiwa siku hiyo ya tukio majira ya saa 2 asubuhi Polisi walipata taarifa toka kwa raia wema kuwa wanafunzi wa chuo cha St. Joseph wanakusudia kuingia ndani ya chuo wakati chuo hicho kilikuwa kimeshafungwa na wanafunzi waliambiwa warejee majumbani kwao.

Kamanda Nsimeki alisema kuwa lengo kubwa la wanafunzi hao inadaiwa ni kutaka uongozi wa chuo hicho hutoe tamko rasmi kuwa ni lini watarejeshwa chuoni kuendelea na masomo yao na madai yao mengine ni kuushinikiza uongozi wa chuo hutengue adhabu waliyokuwa wamepewa raisi wa serikali ya wanafunzi Aristides Mujwahuzi na waziri mkuu wake Deogratius Sanga ambao wamesimamishwa masomo kwa muda wa miezi sita.

Alieleza zaidi kuwa wanafunzi hao wanadai sheria za chuo ni batiri na ni kandamzi ambazo wametaka ziondolewe na mazingira ya vyoo ya chuo hicho ni machafu ambavyo vinahitaji vifanyiwe marekebisho na kutotambua kufungwa kwa chuo hicho.

Alisema kuwa baada ya kuona hali hiyo iliyojitokeza polisi ililazimika kutumia nguvu kidogo ya kupiga mabomu ya machozi kwa lengo la kuwatawanya wanafunzi ambao walikuwa kwenye eneo la chuo na kwamba polisi imefanikiwa kuwakamata wanafunzi 40 walioonekana kukaidi amri ambapo kati yao wanaume wapo 27 na wasichana wapo 13.

No comments:

Post a Comment