Wednesday, January 22, 2014

HAKUNA KAMPUNI YA KITANZANIA IILIYOZUIWA KUWEKEZA KWENYE GESI NA MAFUTA

Dar es Salaam

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete ameeleza kuwa, hakuna Kampuni yoyote ya Kitanzania wala Mtanzania aliyezuaiwa au atakayezuiwa kushiriki katika shughuli za utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi kama ilivyo kwa wawekezaji wengine.

Rais aliyasema hayo jana wakati wa ufunguzi wa Kongamano la Viongozi wa dini waliokutana kwa lengo kutafuta namna bora ya kuelimisha jamii ili kupata elimu na uelewa unaofanana kuhusu namna ya kuziendeleza na kuzisimamia rasilimali za gesi, mafuta na madini pamoja na kuchukua fursa zilizopo huku wakiongozwa na mada kuu isemayo “ Rasilimali zetu za Gesi, Mafuta na Madini kwa Amani na Maendeleo ya Tanzania”.

Alieleza kuwa, kongamano hilo limefanyika katika muda muafaka ambapo gesi na hazina mbalimbali za madini zinagunduliwa nchini, hivyo kuwataka viongozi hao kutafakari namna bora itakayosaidia rasilimali hizo kutumika vizuri kwa manufaa ya Watanzania wote.

Aliongeza kuwa, tayari Tanzania imefanikiwa kupata gesi nyingi isipokuwa bado haijafanikiwa kupata rasilimali ya mafuta na kuongeza kuwa, gesi ni rasilimali kubwa na ikitumika vizuri itaifikisha nchi katika hatua ya juu ya maendeleo na hivyo kuondokana na umasikini.

“Sipendi Tanzania ijute kwa kuwa na rasilimali asilia badala ya baraka iwe balaa. Tusaidieni tusifike huko walikofika wengine kwa ajili ya kuwepo rasilimali hizi. Rasilimali hizi zitufikishe kule tunakotaka kufika, kuboresha maisha ya Watanzania. Alisema Mhe. Rais.

Akizungumzia kuhusu matumizi ya gesi nchini, Mhe. Rais alieleza kuwa, mpango wa Serikali ni kuitumia gesi ndani ya nchi ili pia isaidie kuondoa matumizi ya kuni na mkaa ambayo yamechangia kwa kiasi kikubwa kuharibu mazingira.

“Mpango ni kusambaza gesi kama maji yanavyosambazwa ili wananchi waachane na matumizi ya mikaa na kuni. Tutauza nje lakini si gesi yote itakayouzwa nje, tutaitumia zaidi ndani.” Alisema Rais.

Akizungumzia kuhusu kutengewa maeneo maaalum kwa ajili ya wazawa kushiriki katika uchumi huo, Mhe Rais alieleza kuwa jambo hilo linawezekana lakini lazima ikimbukwe kuwa utaratibu kwa wawekezaji wote ni ule ule wa Serikali kupata kati ya asilimia 65 na 70 na mwekezaji asilimia 30 na35.

“ Tunataka kuliwezesha Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), lakini hata wao wakipewa leseni utaratibu utakuwa ule ule kama wengine na hili ni kwa makampuni yote. Serikali itapata kati ya asilimia 65- 70 na mwekezaji asilimia 30-35. Ndio maana tunapenda hisa ibaki ya Serikali ili rasilimali itunufaishe Watanzania wote”. Alisema.

Kwa upande wake Kiongozi wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) akieleza madhumuni ya Kongamano hilo Askofu DKT. Stephen Munga alieleza kuwa, viongozi wa dini wamekutana na Wizara ya Nishati na kujadili rasilimali hizo kutokana na ukweli kuwa, sehemu kubwa ya shughuli za Wizara hiyo zinagusa mambo ya msingi ya maendeleo ya Taifa.

Aliongeza kuwa, fursa ya kukutana katika kongamano hilo itasaidia kushirikiana na kubadilisha mawazo yatayosaidia kujenga taifa katika kwa amani na nafasi ambayo itawawezesha kutoa taarifa sahihi kwa watanzania wengine kuhusu rasilimali zilizopo na namna wananchi wanavyoweza kuzitumia kwa manufaa yao na ya taifa.

“Tukiwa viongozi wa dini furaha yetu imo kwenye kuona haki ikitendeka, migogoro inamalizika na amani inakuwepo ili watu wa Taifa hili waendelee na shughuli za maendeleo”. Alisema.


Vilevile, alieleza kuwa, nia ya viongozi wa dini ni kuona kwa pamoja changamoto zilizopo kutafuta ufumbuzi kwa pamoja, kusonga mbele katika kutekeleza kwa pamoja waliyokubalina ili kuleta maendeleo tarajiwa.

Wakati huo huo , Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sopspeter Muhongo alieleza kuwa, wizara itaendelea kutekeleza mipango ya kuendeleza uchumi wa gesi kwa maendeleo ya watanzania wote na kuongeza kuwa, Serikali iko tayari kusaidiana na yeyote aliye tayari kuwezeka katika sekta ya gesi na mafuta na kuongeza kuwa, Tanzania itaendelezwa na sekta ya gesi na mafuta.

“Kufika 2025 tunaamini Tanzania itakuwa nchi ya kipato kikubwa. Pato la Taifa litaongezaka na kipato cha mtu mmoja mmoja kitaongezeka na hivyo rasilimali hizi zitatunufaisha wote” Alisema Waziri.

Aidha, aliwataka viongozi hao kuendeleza ushirikiano waliouonyesha wa kutaka kufanya kazi pamoja na wizarakwa manufaa ya Tanzania kuhakikisha rasilimali zilizopatikana zinakuwa na manufaa kwa watanzania wote na vizazi vijavyo.

No comments:

Post a Comment