Mkazi wa kijiji Isagala kata ya Mwamashele wilayani Kishapu mkoa wa Shinyanga ameuawa kikatili baada ya kushambuliwa na wananchi wenye hasira na kisha mwili wake kuchomwa moto akituhumiwa kwa wizi wa kuku wanne.
Hata hivyo mkazi huyo aliyetambuliwa kwa jina la Nganga Shija (22) inadaiwa kabla ya kuuawa kwake alikuwa akikabiliwa na kesi nyingine ya wizi wa kutumia silaha ambapo alikuwa nje kwa dhamana.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Shinyanga, Evarist Mangala alisema tukio hilo lilitokea juzi saa 2.00 asubuhi huko katika kijiji cha Isagala baada ya wanakijiji kumkamata mtuhumiwa huyo akiwa na kuku wanne akihisiwa kuwaiba kutoka kijiji jirani cha Ikonda.
Kamanda Mangala alisema baada ya wanakijiji kumkamata mtuhumiwa huyo na alipohojiwa kuhusiana na kuku aliokuwa nao alishindwa kutoa majibu ya kuridhisha hali iliyosababisha waamue kumshambulia kwa kipigo cha fimbo na mawe hadi kufa na kisha mwili wake waliuchoma moto.
Hata hivyo alisema baada ya kupatikana kwa taarifa za tukio hilo polisi walibaini marehemu alikuwa na kesi nyingine mbili mahakamani zikihusiana na unyang’anyi wa kutumia silaha namba KISH/IR/186/2013 na KISH/IR/188/2013 ambapo kwa wakati huo alikuwa nje kwa dhamana.
“Huyu bwana aliyeuawa inaonekana alikuwa ni mhalifu mzoefu, maana kwa taarifa tulizo nazo kabla ya tukio la juzi pia alikuwa na kesi mbili mahakamani zote hizo alishitakiwa kwa kosa la unyang’anyi wa kutumia silaha ambapo inadaiwa alitumia silaha panga kuwapora baadhi ya wanakijiji,” alieleza Mangala.
Alisema hakuna mtu aliyekamatwa kuhusiana na mauaji hayo ambapo amerejea wito wake wa mara kwa mara wa kuwataka wananchi kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi na kwamba watuhumiwa wote wanaokamatwa wanapaswa kukabidhiwa mikononi mwa dola ili sheria ichukie mkondo wake.
No comments:
Post a Comment