Saturday, January 04, 2014

HII KALI: BAJETI YA MWAKA BUMBULI, ASILIMIA 50 NI MISHARA TU

Lushoto

Baadhi ya Madiwani wa Halmashauri ya Bumbuli wilayani Lushoto mkoani Tanga wameitilia shaka bajeti yao ya mwaka 2014/15 ya sh. bilioni 24.1 kwa kusema haiwezi kuwasaidia kwa vile kati ya fedha hizo sh. bilioni 12.7 ni mishahara, huku fedha za miradi ya maendeleo zikiwa sh. bilioni 9.1.

Akizungumza kwenye Baraza la Madiwani la Bajeti juzi (Ja.2) Diwani wa Kata ya Mponde Richard Mbunghuni alisema halmashauri yao bado mpya, huku ikikabiliwa na changamoto za kukosa barabara za vijijini ili kupitisha mazao ya wakulima, hivyo bajeti hiyo haiwezi kukidhi mahitaji.

"Bajeti hii si ya kuisadia halmashauri kwa vile ni ndogo. Sisi kama halmashauri mpya tuna mambo mengi ambayo tunatakiwa kuyafanya ikiwemo barabara za vijijini ambazo ni muhimu kwa kupitisha mazao ya wakulima wetu, hivyo Serikali ituangalie kama hatubanwi na ukomo wa bajeti" alisema Mbughuni.

Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Lameck Butoto alisema bajeti hiyo wameiongeza kwa kiasi kikubwa, kwani ile ya mwaka 2013/14 ilikuwa sh. bilioni 14.4, lakini pia kwa mapato ya ndani wameruka kutoka sh. milioni 373 2013/14 hadi sh. milioni 619.7 mwaka 2014/15, hivyo anaamini italeta tija.

Akihutubia Baraza hilo, Mkuu wa Wilaya ya Lushoto Alhajj Majid Mwanga alisema halmashauri kutenga fedha asilimia 10 ya mapato yake ya ndani kwa ajili ya mikopo kwa vijana na wanawake sio sadaka bali ni jambo la kisheria, na kuwataka madiwani kulisimamia jambo hilo liweze kutekelezwa.

Akifungua Baraza hilo, Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Amir Shehiza alisema bajeti hiyo isaidie kuimarisha barabara za vijijini ili kusaidia wakulima kupitisha bidhaa zao, lakini pia kuleta ustawi wa jamii kwa matumizi ya fedha hizo kutumika vizuri.


No comments:

Post a Comment