Tuesday, January 07, 2014

HAPA WANANCHI HAWAJAIELEWA EWURA

 Moshi

Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Mjini Moshi (MUWSA), imeiangukia Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), ili kurejesha tozo ya huduma ya majitaka kwa wananchi baada ya kubaini wananchi kufurahia hatua hiyo na kuanza kutupa taka ngumu zinazoharibu mtandao huo.

Imebainika kwamba wananchi hutupa taka ngumu zinazoziba mtandao huo na kuipa kazi ya ziada MUWSA kuizibua huku baadhi ya mitaa majitaka yakianza kutiririka na kuchafua mandhari ya manispaa ya Moshi.

Akizungumza mbele ya waziri wa maji, Profesa Jumanne Maghembe, mkurugenzi wa mamlaka hiyo mhandisi Cyprian Luhemeja alisema tayari ofisi yake imewasiliana na EWURA ili irejeshe tozo hizo ili kujenga nidhamu ya wananchi katika kutumia mtandao huo.

“EWURA imeondoa tozo hili katika agizo lake namba 13-03 la kubadili bei za huduma za majisafi na majitaka za mamlaka lililotolewa Julai 2013 na kuanza kutumika mwezi Agosti 2013” alisema.

Mbali na tozo hiyo, Luhemeja alisema katika siku 180 walizokuwa wamemuahidi waziri, wanatarajia kuongeza makusanyo ya maji kutoka Sh mil 302 ya Juni 2013 hadi sh mil 821 Juni mwaka 2014.

Mipango mingine iliyopo katika utekelezaji ni kupanua mtandao wa maji kwa kuongeza wateja 21,000 hadi wateja 35,000 ifikapo Juni mwaka 2014.

Awali waziri Maghembe,pamoja na kuipongeza MUWSA kwa kuongeza vyanzo vya maji vya Coffee Curing na tankila maji la Kilimanjaro vitavyomaliza tatizo la maji mjini humo,alitaka mgawo wa maji kutorejea mjini humo.

“Mara kadhaa nilikuwa nikisikia kuhusu mgawo wa maji,naomba muhakikishie mgawo wa maji mjini humo uliokuwa ukiripotiwa awali haurejei tena”alisema.


No comments:

Post a Comment