Thursday, December 05, 2013

WAREMBO 15 KUWANIA TOP MODEL TANZANIA


Wanamitindo 15 kutoka mikoa saba, wanatarajia kuwania taji la Tanzania Top Model katika fainali ya mashindano hayo, yanayotarajia kufanyika Jumamosi kwenye Ukumbi mpya wa Mwalimu Julius Nyerere uliopo Mtaa wa Shaaban Robert, Dar es Salaam.

Akizungumza Dar es Salaam juzi, Mratibu wa mashindano hayo, Yusuf Omari ‘Boy George alisema viingilio katika mashindano hayo ni sh. 100,000, sh. 50,000 na sh. 20,000 na tayari tiketi za VIP na Business Class zimeanza kuuzwa.

Mratibu huyo aliwataja washiriki wanaowania taji hilo kuwa ni Ammara, Darline, Nemic, Tina, Maturege, Miracle, Zulpher, Nuru, Lorraine, Iryna, Gladys, Eve, Gaudencia, Niler na Retty.

Alisema mashindano hayo yatakuwa sehemu ya shamrashamra ya kusherehekea miaka 52 ya Tanzania Bara.

Boy George alisema mavazi yatakayotumika ni vazi la Kitanzania (Tanzanian Dress), vazi la kubalizi (Cocktail Dress), vazi la kiofisi (Office Dress) na Vazi la Jioni Evening Dress.

“Pamoja na wanamitindo hawa kushindana katika mavazi, pia watashindana katika vipaji hadi tupate mshindi ambaye atatuwakilisha katika mashindano ya Top Model of the World yatakayofanyika Machi mwakani.

"Tunamshukuru Mungu leo (juzi) ni siku ya 26 wasichana wakiwa kambini na mambo yakiendelea vizuri, ingawa kumekuwepo na changamoto kadhaa kama kuugua kwa baadhi ya Models na upungufu ya vitu vidogo vidogo kutokana na kutokuwepo wadhamini wa kutosheleza mahitaji yote,” alisema.

Alisema mashindano ya Tanzania Top Model yanaendelea kufanyika kwa wananchi kuwapigia kura washiriki.

“Tunaomba wananchi waendelee kufuatilia shughuli za washiriki leo usiku katika vituo vya luninga, ili waone kinachoendelea kwenye kambi na kupiga kura kwa mshiriki anayevutia zaidi.

“Tunahimiza wananchi kupiga kura mara nyingi iwezekanavyo, ili kumfanya mshiriki anayependwa na kupata kura nyingi aweze kushinda. Unachotakiwa kufanya wakati wa kupiga kura ni kutuma ujumbe kwa simu ya mkononi kwenda kwenye Namba 15564 ukiandika TM (unaacha nafasi) halafu jina la mshiriki unayempenda,” alisema.

Alisema mshindi wa Tanzania Top Model atapata zawadi ya fedha taslimu sh. 2,000,000, wa pili na wa tatu kila mmoja sh. 700,000. Jumla.

Mratibu huyo alisema wa nne na wa tano kila mmoja sh. 500,000. Atakayepata kura nyingi za wananchi atapata sh. 1,000.000 na taji la Princess of Tanzania.

“Atakayependeza zaidi katika vazi la Kitanzania atapata sh. 500,000 na taji la Best in Tanzanian Dress na aliyebakia atapata sh.300,000,” alisema

Alisema hadi sasa wadhamini waliojitokeza ni JB Belmont Hotel, For you Boutique, Shear Illusion, NSSF, Tamal Hotel, Primetime Promotion, Screen Masters, TV Tumaini, Nyumbani Lounge, Fabak Fashion, Valye Spring na Rio Gymn.

No comments:

Post a Comment