Hii ni licha ya mahakama kutoa agizo kwa madaktari hao kusitisha mgomo wao ifikapo tarehe 24 Disemba.
Lakini wamesema kuwa wako tayari kuendelea na mazungumzo na serikali kutafuta kusuluhisha kwa mgomo huo unaohusu wao kupokea mishahara yao kutoka kwa serikali za majimbo wala sio serikali kuu.
Jumatano iliyopita waziri wa afya James Macharia alitaka mahakama kutoa agizo la kusitisha mgomo wa madaktari ambao alisema unakiuka katiba na sheria za kazi.
Wagonjwa kote nchini Kenya wameachwa bila huduma za afya kufuatia mgomo wa madaktari na wauguzi ambao umekuwa ukiendelea kwa siku sita sasa.
Hali hii imesababishwa na kutokuwepo maelewano kati ya serikali na chama cha madaktari nchini kuhusu serikali kuamuru madaktari walipwe na serikali za majimbo.
Madaktari wanataka mishahara yao iendelee kulipwa na wizara ya afya kupitia kwa serikali kuu.
Hospitali za umma ndizo zimeathirika zaidi kwani madaktari hawapo kabisa katika hospitali hizo ambapo huduma za afya za serikali sio ghali.
Mgomo huu ulianza wiki jana kwa amri ya katibu mkuu wa chama cha madaktari Sultan Matendechere wakisema wanataka serikali iainishe maswala ya afya chini ya ugatuzi kwenye sheria.
"sheria inashurutisha kuwepo sheria nyingine zinazotoa mwelekeo kuhusu maswala ya afya katika mfumo wa ugatuzi , lakini kwa sasa hilo halifuatwi vilivyo kwani tunatumia sheria za kale mno" alisema Bwana Matendechere.
Chama hicho kinasema kitafanya mgomo wa kihistoria ikiwa serikali haitabatili agizo lake la awali kuwa madaktari walipwe na serikali za majimbo.
Mgomo wa madaktari pia unafanyika katika kipindi ambacho hazina ya malipo ya uzeeni imeongeza kiwango cha mchango cha wafanyakazi hadi asilimia sita, jambo ambalo limewakera mno wafanyakazi katika sekta zote.
TAARIFA HII NI KWA MUJIBU WA BBC SWAHILI
No comments:
Post a Comment