Watu wasiofahamika zaidi ya 15 wamevunja uzio wa Kampuni ya STRABAG kisha kuwakamata walinzi huku wakimuua mmoja na kuweza kuvunja baadhi ya ofisi na kuiba fedha za Kitanzania sh. milioni 56, fedha ya Ulaya (Uero) 450 (sh. 1,080,000) na dola 800 (sh. 1,280,000).
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi jana (Des.21) Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga Constantine Masawe alisema tukio hilo limetokea juzi (Des.20) alifajiri kwenye ofisi za kampuni hiyo zilizopo kijiji cha Kwasunga, kata ya Makuyuni, tarafa ya Mombo wilayani Korogwe.
Masawe alisema watu hao zaidi ya 15 walipoingia waliweza kuwafunga kamba walinzi wawili Ali Mfamanya (30) mkazi wa kijiji cha Kwasunga- Msiga na Suleiman Kamote (50) wa kijiji cha Mashindei kisha kumuua Juma Msami (38) mkazi wa kijiji cha Kwasunga- Mpirani.
Walinzi hao wa Kampuni ya Try Angles Security Service ya Ushirombo, mkoani Geita, walinyang'anywa bunduki mbili na majambazi hao ikiwemo shotgun moja na gobore, ambapo waliingia Ofisi ya Utumishi na kubeba kasiki (sanduku la chuma la kuhifadhi fedha) likiwa na fedha hizo ambazo ni mishahara ya watumishi.
"Baada ya kumuua mlinzi huku wakiwa wamewafunga kamba walinzi wengine waliingia ndani na kuchukua kasiki yenye fedha sh. milioni 56, uero 450 na dola 800, lakini pia walichukua laptop (kompyuta mpakato), printa mbili na passport (hati ya kusafiria) ya nchi ya Austria ya Bw. Flamish" alisema Masawe.
Masawe alisema hadi sasa walinzi hao wanashikiliwa na jeshi la polisi, huku upelelezi na jitihada za kuwasaka watu hao zikiendelea, kwani mazingira ya wizi huo imebidi wafanye hivyo.
Kampuni ya STRABAG inajenga kwa kiwango cha lami barabara kuu ya kutoka Dar es Salaam kwenda Arusha kuanzia kijiji cha Mailikumi wilayani Handeni hadi kijiji cha Mkumbara wilayani Korogwe kilomita 76.
No comments:
Post a Comment