Sunday, December 22, 2013

LEMBELI APOKELEWA KWA KISHINDO JIMBONI KWAKE

Kahama,

Wananchi wilayani Kahama wameipongeza kazi nzuri ya tume ya kamati ya Bunge ya Ardhi , Maliasili na Mazingira baada ya kuanika ukweli juu ya ukiukwaji wa haki za binadamu katika Operesheni Tokomeza Ujangili na kufanya mawaziri wanne kutenguliwa.

Wakiongea katika mkutano wa hadhara jana katika viwanja vya CDT baada ya mapokezi ya mwenyekiti wa kamati hiyo Bw.James Lembeli(Pichani aliyekaa kushoto akiteta na Mh. Harrison Mwakyembe, picha ya library)  ambae ni mbunge wa Kahama walimpongeza kwa kazi nzuri aliyofanya na kamati yake kuwa huo ndiyo uzalendo na kutanguliza maslahi ya nchi yetu.

Awali akiongea Diwani wa Kahama Mjini Bw.Abas Omari ( Chadema ) alimpongeza Bw.Lembeli na kamati yake kuwa wameonyesha uzalendo , huruma kwa wananchi waliofanyiwa ukatiri na manyanyaso na operesheni tokomeza ujangili .

Alisema operesheni hiyo ambayo imewafanya wananchi baadhi kupoteza maisha kupata vilema vya kudumu ikiweomo , mali mbalimbali na mifugo yao iliendeshwa kwa msingi wa kukiuka haki za binadamu.

Mwenyekiti wa halmashauri ya mji wa kahama Bw.Machibya Jidulamabambase alisema kazi iliyofanywa na mbunge Lembeli imewapa faraja waliotendewa mabaya na operesheni tokomeza majangili juu ya ukweli huo ndiyo maana imepelekea mawaziri wanne kuachia ngazi.

Akihutubia mamia ya wananchi katika viwanja vya CDT mbunge Lembeli alisema vitendo vya kinyama vilivyofanywa katika operesheni tokomeza majangili vilikiuka kwa kiasi kikubwa misingi ya haki za binadamu.

Mbunge Lembeli alisema mambo waliyoyabaini baada ya kumaliza kazi ya tume yake katika kufatilia operesheni tokomeza ujangili haikumlenga mtu yeyote lakini hiyo ndiyo hali halisi baada ya kuiwasilisha hayo ndiyo maamuzi ya wabunge na kuwawajibisha mawaziri wanne kwa kushindwa kusimamia.

Ukiukaji wa haki za binadamu juu ya operesheni tokomeza ujangili imepelekea mawaziri wanne kuwajibika ambao ni Waziri wa Mailiasili na Utalii,  Balozi Khamis Kagasheki , Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi Dkt. David Mathayo , Waziri wa Mambo ya Ndani,  Dkt.Emmanuel Nchimbi na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsa Vuai Nahodha.




No comments:

Post a Comment