Saturday, May 25, 2013

MARAIS WA APRM KUCHAGUA MWENYEKITI



Rais Jakaya Kikwete wa Tanzania ni miongoni mwa viongozi 33 wa nchi za Umoja wa Afrika wanachama wa Mpango wa Afrika Kujitathmini Kiutawala Bora (APRM) wanaotarajiwa kuchagua mwenyekiti mpya wa taasisi hiyo Jumapili Mei 26 mjini hapa.

Uchaguzi wa Mwenyekiti wa Wakuu wa Nchi na Serikali za APRM unafuatia kifo cha Mwenyekiti wake, aliyekuwa Waziri Mkuu wa Ethiopia, Meles Zenawi ambaye alipokea kijiti hicho kutoka kwa Mwenyekiti wa kwanza wa taasisi hiyo tangu ilipoanzishwa mwaka 2003, Mzee Olusegun Obasanjo wa Nigeria.


Mwaka 2010 viongozi wa nchi za APRM walikubaliana kuweka ukomo wa wadhifa huo mkubwa katika uongozi na utoaji sera za uendeshaji wa APRM kote Barani Afrika. Kwa mujibu wa muongozo huo, kuanzia uchaguzi wa Jumapili hii, Mwenyekiti atashika madaraka hayo kwa kipindi cha miaka miwili.

Rais Jakaya Kikwete tayari amewasili jijini hapa Ijumaa jioni na Jumamosi amekuwa akikuhudhuria sherehe za miaka 50 tangu kuanzishwa kwa AU. Katika sherehe za Jumamosi Marais wastaafu wa Tanzania, Mzee Alhaji Alli Hassan Mwinyi na Mzee Benjamin Mkapa pia walihudhuria.

Akizungumza katika mahojiano maalum jijini hapa Jumamosi, Katibu Mtendaji wa APRM Tanzania, Rehema Twalib alisema kuna uwezekano wa nchi mbili za Afrika kuwa ndizo zitakazogombea uongozi huo na zitajulikana wakati wa ufunguzi wa kikao hicho.

“Kila kitu tumeelezwa kinakwenda sawa katika maandalizi ya mkutano huo wa uchaguzi na kwa upande wetu tayari tumepata nafasi ya kumpa taarifa Rais Kikwete ikiwa ni maandalizi ya kikao hicho muhimu,” alisema Bi. Rehema.

Uchaguzi wa Jumapili hii unakuja ikiwa ni baada ya viongozi kadhaa wa Afrika akiwemo Rais Jakaya Kikwete, Mark Sall na Jacob Zuma wa Afrika Kusini kutoa hoja ya kufanyika uchaguzi na kutekelezwa sera ya ukomo katika kikao cha Wakuu wa APRM kilichofanyika Januari 26 mwaka huu Addis Ababa.

Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa mjini hapa na makao makuu ya APRM, mbali ya uchaguzi huo wa Mwenyekiti wa viongozi wa APRM, pia mkutano huo utateua Mwenyekiti wa Baraza la Watu Mashuhuri, chombo muhimu katika kuwashauri viongozi wakuu wa nchi za APRM.

Mkutano huo pia utaidhinisha muundo mpya wa Sekretarieti ya APRM makao makuu iliyoko mjini Midrand, Afrika Kusini, unaolenga kukipa chombo hicho cha ngazi ya Bara uwezo zaidi wa kiutendaji kusimamia utekelezaji wa mchakato wa APRM katika nchi 33 wananchama, huku pia nchi hizo zikitarajiwa kuongezeka siku zijazo.



No comments:

Post a Comment