Sunday, March 23, 2014

MTALII NA GUIDE WAKE WAPOTEA KILELE CHA MAWENZI MLIMA KILIMANJARO

Kilimanjaro.

Mtalii mmoja raia wa nchini Ujerumani Jeanne Traska (32) na Athuman Juma muongoza watalii wa hapa nchini, wamekwama katika kilele cha Mawenzi cha Mlima Kilimanjaro.

Kufuatia hali hiyo wahifadhi katika hifadhi ya taifa ya mlima Kilimanjaro KINAPA kwa kushirikiana na kampuni ya utalii ya Nordic ya nchini Kenya wanahaha ili kuweza kuokoa maisha yao.

Jeanne Traska (32) akiwa na muongozaji wake Athuman Juma wanadaiwa kukwama katika mlima huo marchi 22 majira ya saa mbili na nusu asubuhi katika kilele cha Mawenzi kilichopo katika mlima huo mrefu kuliko yote barani Afrika.
Imeelezwa kuwa watu hao walianza kupanda mlima huo marchi 18 mwaka huu wakiongozwa na Kampuni ya Nordic Tours kwa kutumia njia ya Rongai - Kibo –Marangu safari ambayo ingewachukua siku tano.

Kwa mujibu wa Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari ikimnukuu afisa uhusiano wa shirika la hifadhi za Taifa TANAPA Paschal Shelutete ilieleza kuwa watu hao waliamua kupanda kilele cha mlima huo bila kufuata utaratibu wa hifadhi hiyo.

Shelutete alisema kuwa taarifa za awali zinaonyesha kuwa Jeanne alitakiwa kwenda kileleni Kibo lakini katika mazingira yasiyofahamika alibadili uamuzi na kuelekea kilele cha Mawenzi ambacho huwa hakitumiwi na watalii isipokuwa kwa kujaza fomu maalum inayoonyesha kuwa mgeni amekubali kwa hiyari yake kupanda kilele hicho.

“Kwa kawaida mgeni anayepanda kilele cha Mawenzi kilichopo umbali wa zaidi ya meta 4000 kutoka usawa wa bahari hupaswa kuomba ruhusa maalumu kwa hifadhi hiyo lakini cha kushangaza mtalii huyo alibadili safari yake aliyokuwa amearifu awali ya kupanda kilele cha kibo na hivyo kuelekea Mawenzi, ambacho huwa hakitumiwi na watalii isipokuwa kwa kujaza fomu maalum inayoonyesha kuwa mgeni amekubali kwa hiyari yake kupanda kilele hicho”ilisema taarifa hiyo.

Alisema Shirika la Hifadhi za Taifa kwa kushirikiana na Kampuni ya Nordic Tours wanaendelea na jitihada za uokoaji kwa kutumia askari ambao wanaelekea eneo la tukio pamoja na helikopta itakayosaidia zoezi la uokoaji.

Alisema uokoaji huo utategemeana na hali ya hewa itakavyotulia kutokana na kwamba kwa sasa kuna mawingu mazito katika eneo la mlima.

Taarifa zaidi zinasema kuwa kilele cha mawenzi ni kigumu kukifikia kutokana na kuwepo kwa majabali makubwa na miteremko mikali ambayo ni tishio kwa usalama wa wapandaji.

No comments:

Post a Comment