UONGOZI wa klabu ya Simba umemchinjia baharini Kocha wao Mfaransa Patrick Liewig, hivyo mikoba yake itachukuliwa na Kocha na mchezaji wa zamani wa timu hiyo Abdallah King Kibaden.
Kocha huyo Mfaransa aliingia mkataba na Simba Januari 2, Mwaka jana, mkataba wa miezi 18 wa kuifundisha timu hiyo ambapo aliikuta timu hiyo iliwa mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Akizungumza na gazeti hili mmoja wa viongozi wa Simba ambaye hakutaka kuandikwa jina lake gazetini kwa madai kuwa si msemaji wa jambo hilo, alisema kocha huyo Mfaransa uwezekano wa kurudi nchini ni mdogo na badala yake mikoba ya kukinoa kikosi hicho itachukuliwa na Kibaden ambaye msimu uliopita wa ligi alikuwa akiinoa Kagera Sugar na kuiwezesha kushika nafasi ya nne.
"Kwakweli Liewig kurudi sio rahisi na sasa timu inachukuliwa na Kibaden tunaamini na makocha waliokuwepo wataiwezesha timu yetu kufanya vizuri msimu ujao na michuano ya Kombe la Kagame," alisema kiongozi huyo.
Alisema timu yao itaanza mazoezi Jumatano ijayo chini ya Kibaden kwenye Uwanja wa Kines uliopo Shekilango Ubungo,Dar es Salaam kwa ajili ya kujiandaa na Kagame.
Michuano ya kombe la Kagame inatarajiwa kuanza Juni 18, mwaka huu mjini Khartoum nchini Sudan.Simba wapo kundi A na timu za El-Merrekh -(Sudan), APR (Rwanda) na Elman (Somalia) .
Timu zitakazo shiriki mashindano hayo na nchi zinazotokea kwenye mabano ni Al-Hillal, El-Merreikh na Al Shandy (Sudan), Al Nasri (Sudan Kusini), Yanga & Simba (Tanzania), Express (Uganda), Tusker (Kenya), APR (Rwanda), Vitaloo (Burundi), Ports (Djbouti), Elman (Somalia) na Falcon (Zanzibar).

No comments:
Post a Comment