Thursday, June 07, 2012

RWANDA YALAUMU HRW JUU YA VITA VYA DRC

Na mwandishi wetu

WIZARA ya Mambo ya Nje wa Rwanda imelilaumu vikali shirika linalofuatilia haki za binadamu la nchini Marekani la Human Rights Watch (HRW) kwa kutoa habari za upotoshaji kuwa Serikali ya Rwanda inahusika na uchochezi wa vita ya waasi dhidi ya majeshi ya Serikali katika  Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo katika Jimbo la Kivu ya Kaskazini Mashariki mwa nchi hiyo.

Taarifa ya vyombo vya habari iliyotolewa na Wizara ya Nje ya Rwanda kupitia ubalozi wa nchi hiyo jijini Dar es Salaam jana Waziri wa Mambo ya Nje wa Rwanda, Bw. Louise Mushikiwabo, alisema ni jambo la hatari kwa eneo la maziwa makuu iwapo mashirika yasiyo ya kiserikali kama HRW yatapanda mbegu ya uhasama.

“Hatutajali uchokozi kama waliofanya HRW kwa kutumia vigezo vya uongo kama taarifa zilizovuja za Jeshi la kulinda amani la Umoja wa Mataifa  nchini Kongo kudai eti Rwanda imekuwa ikifundisha wanajeshi na kuwatuma DRC kupigana dhidi ya majeshi ya Serikali ya Kinshasa," ilieleza taarifa kwa madai ya taarifa  hizo kuvuja kutoka Jeshi la Umoja wa Mataifa nchini Kongo.

Alisema ni vema taasisi hiyo ya HRW ikaelewa kuwa eneo la maziwa makuu ni eneo ambalo ni kama volcano iliyolala, hivyo kukitokea uchochezi wa aina yeyote linaweza kuleta mlipuko wa machafuko na kuwaathiri wananchi wasio na hatia.

Waziri Mushikiwabo alisema licha ya uchochezi huo wa HRW, lakini Serikali za Rwanda na DRC zimekuwa zikishirikiana kwa karibu ili kupata ufumbuzi wa mgogoro huo uliotokana na waliokuwa waasi wa kikundi cha CNDP ambao waliingizwa katika jeshi la serikali mwaka 2009 baada ya mkataba wa amani kati ya serikali na waasi hao kutoroka jeshini mwishoni mwa mwezi wa tatu na baadaye na kuanza mapambano.

"Kuthibitisha kuwa HRW ina ajenda yake katika kusambaza uongo huo, Waziri Mushikiwabo alisema serikali ya Rwanda inataarifa zote kuwa HRW kwa muda sasa imekuwa ikichangisha fedha toka kwa wahisani mbalimbali ikidai ni kwa ajili ya kuwasaidia waathirika wa mapigano ya mashariki ya DRC na pia kufadhili operesheni zake za kufuatilia masuala ya haki za binaadamu," alisema kupitia taarifa yake.



No comments:

Post a Comment