Thursday, June 07, 2012

RAAWU YASHITAKI UONGOZI WA SHULE KWA WAZIRI

RAAWU yashtaki uongozi
wa shule kwa waziri

CHAMA cha Wafanyakazi wa Elimu ya Juu, Sayansi,Habari na Utafiti (RAAWU) kimemuomba Waziri wa Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana, Bi. Gaudencia Kabaka kuingilia kati mgogoro wa kikazi kati yao na shule ya Kimataifa ya Moshi.

Tamko hilo lilitolewa Dar es Salaam jana na Katibu Mkuu wa RAAWU, Bi.Adelgunda Mgaya, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mgogoro huo na hatua walizochukua hadi sasa.

Bi.Mgaya alisema tamko hilo la kumtaka waziri aingilie kati ni baada ya mgogoro huo kuchukua muda mrefu bila kupatiwa ufumbuzi ili kunusuru ajira na haki za wafanyakazi wanaolazimishwa kujiondoa katika chama hicho.

"Shule hii ilianzishwa mwaka 1969 chini ya uangalizi wa  Hospitali ya KCMC ili kuhudumia watoto wa madaktari na wauguzi na baadaye ilibadili malengo na kupanua wigo ili kuhudumia watu wengi zaidi,
mgogoro huo ulianza tangu mwaka 2009,"alisema Bi. Mgaya.

Alisema baadhi ya mambo yanayohusishwa katika mgogoro huo ni mwajiri kukataa chama cha wafanyakazi kuanzia mwaka 2009.

Kutokana na hali hiyo alisema wafanyakazi walikosa haki yao ya kidemokrasia ndani ya chama kama kufanya vikao vyao vya kutoa elimu, kufanya uchaguzi na kushiriki shughuli zote za chama katika ngazi za juu.

Alisisitiza kuwa mwajiri kukataa kutekeleza mkataba wa hali bora ya maisha tangu mwaka 2008 na kuzuia uongozi wa chama kuingia shuleni hapo ni makosa.

"Shule hii imetushinda kutokana na mambo mengi yakiwemo ya udhalilishaji wafanyakazi yanayodaiwa kufanywa kwa kuwapekua na taarifa tumezipeleka TAMWA) na  Polisi, lakini hakuna hatua zozote zilizochukuliwa,"alisema .





No comments:

Post a Comment