Na mwandishi wetu
ALIYEKUWA mwenyekiti wa Bodi ya wakurugenzi wa Shirika la Usafiri la Dar es Salaam (UDA)Ltd, Bw.Idd Simba na wenzake wawili wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka manane likiwemo la kuipatia hasara UDA ya zaidi ya sh.bilioni 2.378.
Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni aliyekuwa Mkurugenzi wa shirika hilo Bw.Salim Mwaking'inda pamoja na Meneja Mkuu Bw.Victor Milanzi ambapo wote kwa pamoja wanatetewa na wakili Bw.Alex Mgongolwa,Bw.Hely Mally na Bw.Jovin Lymo.
Mbele ya hakimu mfawidhi wa Mahakama hiyo Bw.Ilvin Mugeta,wakili wa serikali kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Bw.Beni Linkon alidai kuwa watuhumiwa hao walitenda makosa hayo katika tarehe tofauti kati ya mwaka 2009 hadi 2011.
Katika shtaka la kwanza,mtuhumiwa Bw.Simba na Bw.Milanzi Septemba 2,2009 ndani ya jiji la Dar es Slaam,kwa pamoja na watu wasiojulikana wanadaiwa kutenda kosa la kuchepusha fedha kinyume cha kifungu namba 29,11 cha sheria ya kupambana na Kuzuia rushwa ya mwaka 2007.
Shtaka la pili ni la kufoji ambapo Bw.Simba na Bw.Milanzi wanadaiwa,Septemba 2,2009 ndani ya jiji la Dar es Salaam walifoji barua ya Septemba 2,2009 kwa lengo la kuonesha kuwa akaunti zote za Benki za shirika la UDA zimeruhusiwa kutoa fedha zaidi ya zilizo kwenye akaunti zao.
Katika Shtaka la tatu washtakiwa hao wanadaiwa Septemba 2,2009,jijini Dar es Salaam,wakiwa kama Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi na Meneja Mkuu wa UDA kwa pamoja wanadaiwa kujichepushia sh.milioni 320 ambazo zilikuwa kama udhamini wa awali na malipo ya hisa za UDA fedha ambazo ziliwasilishwa kwao kwa mujibu wa nafasi zao.
Shtaka la nne watuhumiwa hao wanadaiwa katika tarehe tofauti kati ya Septemba 3,2009 na Machi 31 ,2010 jijini Dar es Salaam,kwa nia ya udanganyifu walijipatia sh.milioni 320 kutoka kwa Bw.Robert Kisena wakijifanya kuwa fedha hizo zilikuwa kama udhamini wa awali na malipo ya hisa za UDA.
Katika shtaka la tano watuhumiwa hao wanadaiwa kati ya Septemba 3,2009 na Machi 31 ,2010 jijini Dar es Salaam wakiwa na nyadhifa zao katika Shirika la UDA,kwa makusudi walijichepushia sh.milioni 320 kwa matumizi yao binafsi fedha ambazo zinadaiwa kulipwa kama udhamini wa awali na malipo ya hisa za UDA kitu ambacho kilisababishia UDA hasara ya kiasi hicho cha fedha.
Shitaka la sita ,watuhumiwa wote watatu wanadaiwa kati ya Septemba 2009 na Februari 2011 jijini Dar es Salaam,wakiwa na nyadhifa zao ndani ya shirika hilo, wakiwa wanatumikiwa nafasi zao,kwa makusudi walitumia vibaya madaraka yao kwa kutoa hisa 7,880,330 za UDA kampuni inayomilikiwa na Serikali Kuu na Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam,kwa thamani ya sh.bilioni 1,142,643,935 bila kuwepo ushindani wa dhabuni kinyume cha sheria ya manunuzi ya umma namba 63 kifungu kidogo cha kwanza.
Shtaka la saba linawakabili washtakiwa wote ambapo wanadaiwa katika tarehe tofauti kati ya Septemba 9 hadi Februari 2011 ndani ya jiji la Dar es Salaam wanadaiwa kwa makusudi kutumia vibaya madaraka yao kwa kufuja hisa 7,880,303 za UDA bila kushirikisha serikali Kuu na Halmashauri ya jiji la Dar es Salaam ambao ni wamiliki wa shirika hilo kitendo ambacho kilikuwa ni ukiukwaji wa sheria ya Muungano wa Makampuni na kifungu cha 74 cha sheria za Makampuni.
Katika shitaka la nane washtakiwa hao wanadaiwa Februari 11,2011 ndani ya jiji la Dar es Salaam,wakiwa kama waajiriwa UDA Ltd wakiwa na nyadhifa zao,kwa makusudi walishindwa kuwa waangalifu kwa kuiuzia Kampuni ya Simon Group Ltd hisa 7,880,303 kwa sh.bilioni 1,142,643,935 bila kutangaza ushindani wa zabuni ambao ungetoa fursa kwa wanunuzi kuweka ushindani wa bei kwa hisa husika kitu ambacho kimeisababishia UDA hasara inayotazamiwa kufikia sh.bilioni 2,378,858,878.80 kama faida bora ambayo kampuni hiyo ingeipata.
Watuhumiwa hao wote walikana kutenda makosa hayo ambapo upande wa mashitaka ulidai kuwa upelelezi wa shauri hilo umeshakamilika na kuomba tarehe ya kutajwa kabla ya kupangwa tarehe ya kuwasomea watuhumiwa hao maelezo ya wali.
Katika hatua nyingine ,upande wa jamhuri ulidai kuwa hauna pingamizi na dhamana kwa watuhumiwa wote ambapo hakimu Bw.Mugeta alisema watuhumiwa hao watadhaminiwa kwa kusaidi bondi ya sh.milioni 500 kila mmoja pamoja na kuwa na wadhamini wawili.
Alisema kuwa dhamana hiyo itaenda sambamba na washtakiwa kuweka hati ya mali isiyohamishika ambapo watuhumiwa wote kwa pamoja waliweka hati ya Kampuni ya Bw.Simba yenye thamani ya sh.bilioni 8 na kufanikisha udhamini wao.
Habari nje ya Mahakama zilidai kuwa Kampuni ya Simon Group Ltd ni miongoni mwa watu wataokuja kutoa ushahidi dhidi ya Bw.Simba pindi kesi itakapoanza kusikilizwa
Kesi hiyo itatajwa tena Juni 28 mwaka huu,watuhumiwa wote wapo nje kwa dhamana.

No comments:
Post a Comment