Thursday, June 07, 2012
CHADEMA WAZINDUA M4C KWA KISHINDO "WADAI CCM NI CHEPESI KAMA KARATASI
Na mwandishi wetu
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), jana kimezindua kampeni yake ya (Movement For Change M4C), mkoani Mtwara kwa kishindo na kuwataka wananchi mkoani hapa kukikataa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wakidai chama hicho kwa sasa ni chepesi kama karatasi.
Uzinduzi huo ulifanywa na Mwenyekiti wa chama hicho Taifa, Bw. Freeman Mbowe katika mkutano wa hadhara ambao ulihudhuriwa na umati mkubwa wa watu na kusisitiz akuwa, wakati wa kuibeba CCM umekwisha kwani chama hicho kimechangia matatizo yanayowakabili wananchi na hakina nguvu tena ya kutawala.
“Askari wangu tunawaheshimu sana, wapo wanaofanyakazi kwa amri…ukipewa amri changanya na akili zenu maana mnaowapiga leo ndiyo watakaokuwa watawala wenu,” alisema Bw. Mbowe na kudai kushangazwa na wananchi mkoani hapa kuchagua wabunge wasio na sifa za kuwa wawakilishi wao.
Alisisitiza kuwa, Watanzania wamechoka kucheka na watawala wakati watu wanakufa kwa kukosa dawa ambapo mapokezi ya chama hicho, yalivunja dhana ya kwamba, mikoa ya Kusini ambayo ni Mtwara na Lindi ni ngome ya CCM na CUF.
Mkutano huo ulifanyika chini ya ulinzi mkali wa Jeshi la Polisi waliokuwa wakizunguka na kuleta hofu kwa wananchi hivyo kusababisha Mwenyekiti wa Baraza la Vijana Taifa (BAVICHA), John Heche kuwaondoa hofu.
Bw. Heche ambaye ni Kamanda wa Oparesheni ya “Vua Gamba, Vaa Gwanda” katika mikoa ya Kusini, alilazimika kusimama na kuwashambulia askari kwa kuwataka waache vihelehele vya kuwatisha wananchi na kuwatetea viongozi wa CCM.
Kauli ya Bw. Heche iliufanya umati wa wananchi waliokuwa wamefurika katika mkutano huo kushangilia, kuwazomea polisi ambao walidai ndiyo kikwazo cha maendeleo mkoani humo.
“Polisi acheni kihelehele, mabosi wenu wako CCM lakini nyie msio na bega, mnasota na maisha kama tulivyo CHADEMA, naombe wananchi msiwe na wasiwasi wapo hapa kwa ajili yetu kutulinda.
“CHADEMA hatuna sababu ya kulindwa na polisi, mikutano yetu inalindwa na nguvu ya umma ambayo ni wananchi wenyewe, naomba tuachane na CCM ambayo imeshindwa kutatua kero zenu badala yake wamejimilikisha rasilimali za nchi.
“Barabara zote ni mbovu, leo tunashuhudia CCM wamefunga ndoa na CUF, nao ni magamba wanaotakiwa kuvua na kuvaa gwanga,” alisema.
Aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM, Mkoa wa Arusha, Bw. Ally Bananga, alisema Serikali imeshindwa kuweka mikakati ya kuwakomboa wananchi.
“Kinachofanyika ndani ya CCM ni kuziba shimo la panya kwa kutumia mkate ambao hamzuii kupita,” alisema.
Kwa Upande wake, aliyekuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), mkoani Arusha, Bw. James Millya, alisema watanzania wamegawanywa katika makundi mawili ya wenye nacho na wasio nacho.
“Zipo sababu za kuiondoa Serikali ya CCM madarakani kwa sababu
imeshindwa kutatua matatizo ya wananchi kwa muda muafaka, leo sitafananua kila kitu lakini pimeni nyie wenyewe, wananchi wa Arusha, Dar es Salaam na Mwanza ulinganishe na wakazi wa Mtwara,” alisema Bw. Millya.
Alisema CCM itaondolewa madarakani kwa nguvu ya umma na kusulubiwa na sauti za wananchi hivyo aliwataka waungane kuikataa na kuiondoa madarakani.
Mbunge wa Singida Masharikia, Bw. Tindu Lissu, alisema mikoa ya Lindi, Mtwara na Singida ni ya mwisho kutengewa bajeti ndogo na Serikali lakini iko mstari wa mbele kuichagua CCM.
“Hata bejeti ya mwaka huu itakuwa hivyo, si kwamba mikoa hii ina mahitaji machache bali ni kushindwa kufikia vigezo vya kimataifa vya maendeleo vilivyowekwa,” alisema.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)

No comments:
Post a Comment