Thursday, March 22, 2018

MALAWI YAVUTIWA NA MATIBABU YA KIBINGWA MOI


Na Mwandishi Wetu

Katibu Mkuu Wizara ya Afya ya Malawi Dkt. Charles Mwansambo ametembelea Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI) ili kupata uzoefu wa namna Taasisi hiyo inavyotoa huduma za kibobezi (super specialist).

Akizungumza wakati wa ziara hiyo leo Jijini Dar es Salaam Dkt. Mwansambo amesema ametembelea MOI ili kuona uwezekano wa kuwaleta wagonjwa wa Malawi kupata huduma za Kibingwa za Mifupa, Upasuaji wa Ubongo, Mgongo na Mishipa ya fahamu badala yakuwapeleka India.

" Nimefurahi kuona kuwa tuna huduma nzuri za kibingwa kwa jirani zetu wa Tanzania, hili ni jambo jema na litatupunguzia gharama za kuwapeleka wagonjwa India badala yake tunawaleta hapa MOI" amesema Dkt.Mwansambo.

Aidha, Dkt. Mwansambo alipata fursa ya kutembelea vyumba vya upasuaji vya MOI, vyumba vya wagonjwa walioko katika uangalizi maalum (ICU), wodi za watoto na wodi maalum za kisasa za kulipia.

Kutokana na mafanikio ya miundo mbinu ya kisasa yaliyopo MOI Dkt. Mwansambo ameonyesha dhamira ya dhati ya kuleta madaktari wanafunzi hapa ili wapate ujuzi wa zaidi.

Naye, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa MOI Mhandisi .Reginald Kimambo alimueleza Dkt. Mwansambo kwamba huduma zinazotolewa katika hospitali hiyo zimebobea katika Mifupa, Ajali, Upasuaji wa ubongo, mgongo, mishipa ya fahamu pamoja na kutua mafunzo kwa madaktari bingwa wa COSESCA.

Ziara hii imekuja baada ya mkutano wa 65 wa Mawaziri wa Afya wa Ukanda wa Afrika Mashariki, Kati na Kusini uliofanyika Jijini Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment