Tuesday, August 09, 2016

MFUMUKO WA BEI WA TAIFA WA MWEZI JULAI 2016 UMEPUNGUA HADI ASILIMIA 5.1.


  Mkurugenzi wa Sensa na Takwimu za Jamii wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Ephraimu Kwesigabo (kulia) akitangaza Mfumuko wa Bei wa Taifa wa mwezi Julai, 2016 ambao umefikia asilimia 5.1 kutoka asilimia 5.5 za mwezi Juni 2016.Kushoto ni Kaimu Meneja wa wa Idara ya Takwimu za Ajira na Bei wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Bi. Ruth Minja.
Baadhi ya waandishi wa Habari wakifuatilia taarifa ya Mfumuko wa Bei wa Mwezi Julai, 2016 iliyokuwa ikitolewa na Mkurugenzi wa Sensa na Takwimu za Jamii wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Ephraimu Kwesigabo leo jijini Dar es salaam. 


Na. Aron Msigwa – Dar es salaam.

OFISI YA TAIFA YA TAKWIMU (NBS) imetangaza mfumuko wa Bei wa Taifa wa mwezi Julai 2016 na kueleza kuwa umepungua hadi kufikia asilimia 5.1 kutoka asilimia 5.5 iliyokuwepo mwezi Juni mwaka huu.

Akitangaza taarifa ya mfumuko wa Bei wa Taifa wa mwezi Julai, 2016 leo jijini Dar es salaam, Mkurugenzi wa Sensa na Takwimu za Jamii wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Bw. Ephraimu Kwesigabo amesema kuwa kasi ya upandaji wa bei ya bidhaa na huduma kwa mwaka ulioishia mwezi Julai, 2016 imepungua ikilinganishwa na kasi iliyokuwepo kwa mwaka ulioishia mwezi Juni 2016.

Ameeleza kuwa kupungua kwa mfumuko wa Bei wa mwezi Julai 2016 kumechangiwa na kupungua kwa kasi ya bei ya baadhi ya bidhaa za vyakula na zile zisizo za vyakula kwa kipindi kilichoishia Julai 2016 zikiwemo bidhaa za samaki kwa asilimia 6.6, mafuta ya kupikia asilimia 4.9 na maharage kwa asilimia 1.9 huku bei zisizo za vyakula zikihusisha  ni gesi kwa asilimia 21.5, mafuta ya taa 9.4 na dizeli kwa asilimia 10.3.

Kwa upande wa bidhaa zisizo za vyakula zilizoonesha kupungua bei ni pamoja na bidhaa za gesi kwa asilimia 21.5, mafuta ya taa kwa asilimia 9.4 na dizeli kwa asilimia 10.3.

Aidha, ameeleza kuwa pamoja kupungua huko, kasi ya upandaji wa bei ya bidhaa na huduma kwa mwaka ulioishia mwezi Julai, 2016 kwenye baadhi ya bidhaa umeonesha kuongezeka katika kipindi hicho hasa kwenye kama  mchele, mahindi, unga wa mahindi, vyakula kwenye migahawa na mkaa.

Bw. Kwesigabo amesema kuwa Fahirisi za Bei nazo zimeongezeka hadi kufikia 103.50 mwezi Julai, 2016 kutoka 103.47 za mwezi Juni 2016, ongezeko  ambalo limechangiwa na kuongezeka kwa bei ya baadhi ya bidhaa za vyakula zile  zisizokuwa  za vyakula.

Amesema ongezeko hilo la Fahirisi linahusisha kundi la bidhaa na huduma za vyakula na vinywaji baridi, Vinywaji vyenye kilevi na bidhaa za Tumbaku, Mavazi ya nguo na viatu, nishati, maji na Makazi pamoja na Samani, vifaa vya nyumbani na ukarabati wa nyumba.

Kundi lingine linahusisha gharama za Afya, usafirishaji, Mawasiliano, Utamaduni na Burudani, Elimu, hoteli na migahawa pamoja na bidhaa na huduma nyinginezo ambazo jumla ya Fahirisi za Bidhaa hizo kwa mwezi huo zimefikia 103.50.

“Baadhi ya bidhaa zilizo sababisha kuongezeka kwa Fahirisi ni pamoja na mafuta ya kupikia asilimia 1.1, samaki wabichi asilimia 6.0, matunda asilimia 4.9, maharage makavu kwa asilimia 2.7, ndizi za kupika asilimia 1.9 na mahindi kwa asilimia 1.5” Amesisitiza Kwesigabo.

Mbali na hilo ameeleza kuwa Mfumuko wa Bei wa Bidhaa za vyakula na vinywaji baridi kwa mwezi Julai 2016 umepungua hadi kufikia asilimia 7.6 kutoka asilimia 8.1 ya mwezi Juni 2016.

Kwa upande wa uwezo wa shilingi ya 100 ya Tanzania katika kununua bidhaa na huduma umefikia shilingi 96 na senti 62 mwezi Julai 2016 ikilinganishwa na shilingi 96 na senti 65 ya mwezi Juni, 2016.

Aidha, hali ya Mfumuko wa Bei kwa baadhi ya nchi za Afrika Mashariki imeonesha kuwa nchi ya Kenya Mfumuko wa Bei wa mwezi Julai umeongezeka hadi kufikia asilimia 6.39 kutoka asilimia 5.80 za mwezi Juni, 2016, Uganda ikiwa na Mfumuko wa Bei uliopungua wa asilimia 5.1 kwa mwezi Julai kutoka asilimia 5.9 za mwezi Juni, 2016.




No comments:

Post a Comment