Mkuu wa Mkoa wa Simiyu , Mhe. Anthon Mtaka akizungumza na wakazi wa Kijiji cha Mwamgoba wilayani Busega (hawapo pichani) kabla ya zoezi la uhawilishaji fedha za ruzuku kwa wanufaika wa Mpango wa kunusuru kaya maskini TASAF III kijijini hapo, Wilayani Busega Mkoani humo.
Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu, Bw. Jumanne Sagini akifafanua jambo kwa wakazi wa Kijiji cha Mwamgoba wilayani Busega (hawapo pichani) kabla ya zoezi la uhawilishaji fedha za ruzuku kwa wanufaika wa Mpango wa kunusuru kaya maskini TASAF III kijijini hapo, Wilayani Busega Mkoani humo.
Na Stella Kalinga (Ofisi ya Mkoa wa Simiyu)
Mkuu wa mkoa wa Simiyu Mhe. Anthony Mtaka amewataka viongozi wa kata na vijiji kuwabaini wanufaika wa Mpango wa kunusuru kaya TASAF III(PSSN) wanaojihusisha na ulevi na kuwaondoa katika orodha ya wanufaika wa mpango huo.
Mtaka ametoa agizo hilo wakati alipozungumza na wananchi wa kijiji cha Mwamgoba wilayani Busega katika zoezi la uhawilishaji fedha za TASAF III PSSN, ambapo jumla ya shilingi 2,976,000 zimegawiwa kwa wanufaika 82 kijijini hapo.
Mtaka amesema lengo la mpango wa TASAF III ni kuwatoa watanzania katika hali ya umaskini kwa kuwapa ruzuku itakayowasadia kupata huduma muhimu ikiwa ni pamoja huduma za afya, kuwasaidia watoto wao waweze kwenda shule lakini baadhi ya wanufaika wamekuwa wakitumia fedha hizo kulewa badala ya kuanzisha miradi midogo midogo kama ufugaji wa kuku, mbuzi na kondoo pamoja na kilimo ili miradi hiyo iwasaidie kuwaongezea kipato.
“Hatuwezi kuleta fedha tukifikiri zitawasaidia kujikwamua katika Umaskini lakini mnashinda baa na vilabuni kulewa , wengine mnaongeza wake, tukiwabaini mtaondolewa kwenye huu mpango” , alisema Mtaka.
Mtaka amewataka wanufaika hao kujishugulisha na kilimo na ufugaji na kuondokana na dhana ya kuwa watakuwa wanufaika wa mpango huo siku zote, ambapo alieleza azma ya Serikali ya awamu ya tano ya kuwatoa wananchi katika umaskini na kuwaondolea changamoto mbalimbali kama kutoa elimu ya bila malipo na kuanzisha Mfuko wa Huduma ya Afya Watanzania wasio na uwezo waweze kupata matibabu kwa gharama nafuu na akatoa wito kwa wanufaika hao kujiunga na Mfuko wa Huduma ya Afya ya Jamii (CHF)ambao utawasaidia wao wenyewe pamoja na wategemezi wao kupata huduma za Afya katika Vituo vya kutolea huduma za Afya.
Aidha, ametoa wito kwa wazazi kuwakumbusha watoto wao wajibu wa kuwatunza kwa sababu kumekuwa na baadhi ya wazee ambao wametambuliwa kuwa ni maskini, wakati wana watoto wenye nguvu na uwezo wa kuwasaidia lakini hawatimizi wajibu wao kuwatunza kwa kuwapa mahitaji muhimu.
Akizungumza baada ya kukabidhiwa fedha hizo Bibi. Christina Robert ambaye ni mnufaika wa mpango wa TASAF amesema mpango huo umemsaidia kuondokana na kuishi katika nyumba ya nyasi na matope na kumuwezesha kujenga nyumba ya matofali na bati.
“Naishukuru TASAF maana imenisaidia sana, ruzuku niliyopewa mara ya kwanza ilinisaidia kutibiwa nilipofanyiwa upasuaji, mara ya pili nilitumia tena kwenye matibabu, mara ya tatu nilinunua kuku na bata, mara ya nne nikanunua bati nikajenga nyumba ya vyumba viwili”, alisema Christina.
Pamoja na kusisitiza juu ya matumizi sahihi ya fedha za ruzuku za TASAF Mtaka amewataka wananchi wa Busega na Mkoa wa Simiyu kwa ujumla kuongeza juhudi katika kilimo cha mazao ya mikunde kwa kuwa tayari Serikali ya India imekubali kununua zaidi ya tani milioni sita ya choroko, dengu na mbaazi kutoka Tanzania, hivyo wakati utekelezaji wa makubaliano hayo utakapoanza wananchi walime kwa wingi mazao hayo kwa kuwa kutakuwa na soko la uhakika.
Jumla ya kaya 4260 zilibainishwa katika vijiji 41 vya wilaya ya Busega ambapo kaya 53 ziliondolewa katika mpango wa TASAF III PSSN baada ya uhakiki na kubaini kuwa hazikukidhi vigezo.
Baadhi ya wanufaika wa Mpango wa kunusuru kaya maskini TASAF III katika kijiji cha Mwamgoba Wilayani Busega, wakiwasikiliza Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka na katibu tawala Jumanne Sagini (hawapo pichani), walipozungumza nao kabla ya zoezi la uhawilishaji wa fedha za ruzuku kwa ajili ya mpango huo.
Bw. Methesela Mrobi akimuonesha Mkuu wa Mkoa wa Simiyu na viongozi wengine wa Mkoa na Wilaya(hawapo pichani) Bwawa dogo alilochimba kwa kutumia fedha za ruzuku za Mpango wa kunusuru kaya maskini TASAF III, ambalo analitumia kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji
Mkuu wa Wilaya ya Busega , Mhe. Tano Mwera (katikati) na Katibu Tawala Wilaya ya Busega, Bw. Sebastian Masanja (kulia) wakizungumza jambo kabla ya zoezi la uhawilishaji fedha za ruzuku kwa wanufaika wa Mpango wa kunusuru kaya maskini TASAF III kijiji cha Mwamgoba, Wilayani Busega (kushoto) Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu, Bw. Jumanne Sagini
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu , Mhe. Anthon Mtaka akimkabidhi fedha Bw. Methesela Mrobi wakati wa zoezi la uhawilishaji fedha za ruzuku kwa wanufaika wa Mpango wa kunusuru kaya maskini TASAF III ,katika kijiji cha Mwamgoba, Wilaya ya Busega Mkoani humo.
No comments:
Post a Comment